ALIYEKUWA kiongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Algeria, Rweikiza Rugeyamba ametia ndani Dola za Marekani 12,539.32 (zaidi ya Sh milioni 18) zilizotolewa na
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa ajili ya wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini humo.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa Jumatano bungeni mjini Dodoma, ilieleza kuwa fedha hizo za wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini Algeria, zilipelekwa kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa mnamo Aprili 2009.
Fedha hizo zilikuwa ni za kujikimu kwa wanafunzi watano. “Hata hivyo; tulibaini kuwa fedha hizo hazikuwa zimelipwa kwa wanafunzi hao kama ilivyokusudiwa,” inasema sehemu ya
ripoti ya CAG, Ludovick Utouh.
Rweikiza anadaiwa kutia ndani fedha hizo baada ya kulipwa na Ubalozi wa Ufaransa kupitia akaunti Namba 0163300019/68 ambayo mmiliki wake ni Rweikiza Rugeyamba ambaye
alikuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini Algeria kwa lengo la kuwapatia wenzake waliokusudiwa.
CAG katika ripoti hiyo anasema Rugeyamba alipunguza kiasi cha fedha katika fedha alizotakiwa kuwapatia wanafunzi wenzake na kuwaacha wakiishi maisha magumu.
Pia, Rweikiza anadaiwa kutumia fursa ya kuaminiwa na wenzake kwa kutayarisha orodha ya malipo bandia na kuacha kiasi cha zile fedha zilizotumwa kwake kutoka Ubalozi wa nchini
Ufaransa kwa kupunguza viwango vilivyotayarishwa na Bodi ya Mikopo.
Inadaiwa kuwa Februari 2009, HESLB ilituma Dola za Marekani 35,644.11 (Sh milioni 46.9), lakini Rweikiza alitayarisha orodha nyingine iliyopunguzwa Dola 70.25 ambayo ni fedha
aliyojipatia visivyo halali. Hata hivyo, Rweikiza alishasimamishwa masomo Algeria na alisharudishwa nchini na uchunguzi wa Polisi unaendelea.
CAG katika ripoti hiyo pia amebainisha kuwa ukaguzi walioufanya katika nchi za India, Russia na China ulibaini kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wamekuwa wakilipwa na Bodi ya Mikopo ada na posho za malazi bila ya kupata na kupitia taarifa za maendeleo ya kitaaluma.
“Haikuweza kufahamika ni kwa namna gani na ni kwa vigezo vipi ambavyo Bodi ya Mikopo inaweza kutoa mikopo katika mazingira haya wakati kunakuwa na wanafunzi wengine wanaofeli mitihani yao na wengine kufukuzwa vyuo?” alihoji CAG.
Alitoa mfano kuwa nchini China mwanafunzi anayejulikana kwa jina la Magimila Shamoro Ahmad wa Chuo Kikuu cha Afya cha Tianjian alifeli masomo na kuondoka chuoni baada ya
kupokea kiasi cha Sh milioni 12.5 kama mkopo wa masomo kutoka Bodi ya Mikopo.
CAG katika ripoti hiyo ameeleza kuwa kutoka mwaka 1994 hadi Juni 2009, Bodi ya Mikopo ilikuwa imetoa jumla ya mikopo inayofikia Sh bilioni 433.3 kwa wanafunzi katika vyuo
mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo kati ya mikopo hiyo, Sh bilioni 80.9 ni mikopo inayotakiwa kurejeshwa.
0 Comments