KADA mkongwe wa CCM ambaye pia ni Kamanda wa Vijana wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru, amesema Tanzania inakabiliwa na ugonjwa mbaya wa ubinafsi unaosababisha watu wake kugombea uongozi.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wakati akielimisha vijana wa CCM wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kada huyo alisema ingawa ugonjwa huo upo katika nchi nyingi za Afrika, kwa Tanzania umekithiri.

Kwa mujibu wa Kingunge, tofauti na ilivyokuwa kwa waasisi wa Uhuru na Muungano walioupa uzalendo kipaumbele na kuhakikisha maendeleo ya nchi, viongozi wengi sasa wanaendekeza zaidi ubinafsi na kuishia kugombea vyeo badala ya kushirikiana na wananchi kuendeleza nchi. “Huu ni ugonjwa mbaya, wa aibu na usioruhusu busara.

Ulizuka muda mfupi baada ya Uhuru na Muungano kuleta marupurupu na maslahi kwa wanaoongoza … zamani hapakuwa na mambo haya, hakuna aliyethubutu kugombea uongozi na kila mmoja alijaribu kwa uwezo wake na kwa kushirikiana na wenzake kuhakikisha kuwa nchi inapata maendeleo,” alisema.

Alifafanua kuwa siku hizi watu wanachafuana na kunyoosheana vidole kwa sababu ya uongozi, huku wakitambua kuwa wanachokifuata katika madaraka hayo ni maslahi binafsi na wala si maendeleo ya nchi, jambo linalouthibitishia umma kuwa wana udhaifu.

Katika hatua nyingine, kada huyo aliwabeza wanaohoji uwepo wa Muungano na kusema wana lao jambo na wamepungukiwa busara.

Alisema, “tena ni marafiki zangu, maprofesa na wasomi, wanaanzisha mada eti kuhoji umuhimu wa Muungano, tena wanasema eti ulikuwa ni uamuzi wa Mwalimu Nyerere na Abeid Amaan Karume pekee, jamani na usomi wao wote hawajui kuwa hao walikuwa marais na waliwawakilisha wananchi? Wapuuzeni”.

Pia aliwataka vijana nchini kujifunza historia yao ili wasije wakadanganywa, kupotoshwa na kutumiwa kuwa chanzo cha matatizo nchini baadaye.

Lakini mwishoni mwa wiki katika kipindi cha Kipima Joto cha ITV, mchangia mada kutoka CUF, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Julius Mtatiro, alisisitiza hoja ya vyama vya
upinzani ya siku nyingi ya kutaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu badala ya serikali mbili zilizopo.

Hata hivyo, mchangia mada mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, aliwashangaa watu wanaotaka kurudishwa kwa Tanganyika huku wakisema wanawaenzi waasisi wa Muungano na kukubaliana na suala la Muungano wa Afrika.

Dk. Lwaitama alihoji kama wanasiasa hao wanakubaliana na wazo la kuwa na Serikali ya Afrika, kwa nini wanaifufua Tanganyika, ambayo haipo na hata wananchi wengi wa sasa wameishi miaka mingi kama Watanzania?

Pia msomi huyo aliwashangaa wanatoa hoja hizo huku wakisema kuwa Serikali iliyopo ina
mawaziri wengi, akahoji, watapunguzaje mawaziri wakati wanataka kuwe na serikali ya tatu?

Aliwalaumu wanasiasa hasa kutoka CCM kwa kushindwa kujenga hoja za kutetea mfumo wa serikali mbili na kuacha watu kujitokeza na upotoshaji ukiwamo wa kuifufua Tanganyika na hoja ya serikali tatu.

Alisema Zanzibar ndio wanaostahili kuwa na serikali katika Muungano kwa kuwa wana haki ya
kuwa na uoga wa kumezwa tofauti na Tanzania Bara ambayo haiwezekani kabisa kumezwa na Zanzibar.

Alitoa mfano wa Muungano wa Uingereza ambao unajumuisha England, Wales na Scotland, na kufafanua kuwa England haijawahi kufikiria kuwa na serikali kwa kuwa haiwezi kumezwa na Scotland wala Wales ambazo zina serikali.

Akihojiwa na kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1) Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Samuel Mushi alisema kuna utafiti ambao ulifanywa na Mpango wa Utafiti wa Demokrasia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Redet), ukaonesha kuwa ni asilimia tisa tu ya Wazanzibari wanaotaka Muungano uvunjwe na wengi wao ni wanasiasa.

Kwa mujibu wa Profesa Mushi, utafiti huo ulibainisha kuwa wananchi wa kawaida Visiwani wanataka mfumo wa serikali mbili uendelee, kwani unaipa Zanzibar kuwa na serikali yake. Hata hivyo, alisema Wazanzibari hawataki kuundwa kwa serikali moja kama inavyopendekezwa na baadhi ya watu.

Kuhusu manung’uniko yanayojitokeza kuhusu Muungano, Profesa Mushi alisema vijana wengi hawataki Muungano, kutokana na usiri uliogubika namna mambo 22 yalivyofikiwa na kuyafanya kuwa masuala ya Muungano.

Alisema kitendo cha Serikali kutoweka wazi namna ilivyoyaingiza mambo hayo na kitendo cha kuyajadili chini kwa chini kwa kisingizio kuwa ni masuala nyeti, ndio yanayofanya vijana sasa kuhoji mambo hayo kwa jazba.

Alisema vijana wengi wakati wa Muungano walikuwa hawajazaliwa sasa hivi wanatakiwa waelimishwe kwa undani juu ya mambo yaliyoko katika Muungano.

Alionya kuwa bila kufanya hivyo, vijana wengi watasombwa na fikra za watu ambao hawataki Muungano na ndio maana mijadala mingi ya suala hilo inatawaliwa na jazba hasa kwa Zanzibar.

Hata hivyo, Profesa Mushi aliwataka vijana kuzungumza mambo ya Muungano kistarabu bila
jazba na wahusika.

Alikiri kuwa upande wa Zanzibar wana malalamiko mengi, lakini akawaasa wasitumie jazba kwenye mijadala.

“Tanzania tunahitaji Muungano huu na pia tunahitaji shirikisho la Afrika Mashariki, dunia ina changamoto nyingi, ni vyema watu wakaungana na kuwa na nguvu,” alisema Mushi.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Idd, alikiri kuwa bado kuna kero katika Muungano lakini SMZ inapoona kuwa kuna suala ambalo likiondolewa kwenye Muungano lina faida kwa Zanzibar, wamekuwa wakifanya hivyo kwa kufuata utaratibu.

“Kama tulivyoona suala la mafuta kuwa liondolewe kwenye Muungano, tunachofanya sasa ni kuomba kwa utaratibu uliopo. Lengo letu Muungano huu uwe wa maslahi ya wananchi wote,” alisema Balozi Idd.

Hivi karibuni, baadhi ya wananchi wa Zanzibar wakati wa kujadili Muswada wa Marekebisho ya Katiba walipandwa na jazba hadi kuuchana Muswada huo kwa madai kuwa hauoneshi masuala ya Muungano.

Wengi wa watu hao walisikika kwa uwazi wakisema kuwa hawautaki Muungano, kwani visiwa hivyo vimerudi nyuma kimaendeleo kutokana na kukandamizwa na Bara.