Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anakutana na Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi kujadili kuhusu suala tete la wakimbizi kutoka Afrika Kaskazini.
Ufaransa haijafurahishwa na hatua ya Italia kuwapa viza maelfu ya wakimbizi, hivyo kuwapa uhuru wa kuingia nchi yoyote ya Ulaya kutokana na mkataba wa Schengen.
Karibu wakimbizi 25,000 wameingia kusini mwa Italia mwaka huu wengi wao wakiwa ni matokeo ya machafuko ya kisiasa yaliyotokea Afrika Kaskazini.Wengi wa hao ni wakimbizi kutoka Tunisia na wanataka kuungana na ndugu zao wanaoishi Ufaransa.
Maafisa wanasema ni matarajio ya wengi kuwa kupitia mkutano wao mjini Rome, Rais Sarkozy na Waziri Mkuu Berlusconi wataweka pembeni tofauti zao na kukubaliana na kupeleka mapendekezo ya pamoja mjini Brussels, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC.
Kati ya mambo yanayojadiliwa ni njia za kudhibiti mipaka iwapo machafuko ya kisiasa yataendelea kuleta wakimbizi zaidi.
Ufaransa 'haihitaji kusitisha mkataba wa Schengen kwa muda' lakini, 'kupitia vipengele vinavyosimamia baadhi ya mazingira,' alisema Henri Guaino, mshauri maalum wa Rais Sarkozy, akinukuliwa na shirika la habari la AFP.
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Franco Frattini amesema makubaliano ya Schengen ni 'moja ya nguzo muhimu za Ulaya ikiwemo Euro ambazo haziwezi kuhojiwa kuwepo kwake.'
Lakini akaongeza kuwa udhibiti wa aina fulani unaweza kuwekwa kuhakikisha makabaliano yanaendana na hali halisi ya sasa.
Makubaliano ya Schengen yanaruhusu wakazi halali wa nchi nyingi za Ulaya Switzerland, Norway na Iceland kuingia kwa masharti machache tu.
0 Comments