Jeshi la polisi kanda maalum ya Tarime na Rorya katika mkoa wa Mara, limewatia mbaroni wakazi wawili wa wilaya ya Tarime kwa kukutwa na tani 4.5 za bangi kavu wakiwa katika maandalizi ya kuisafirishwa kwenda nchi jirani ya Kenya.
Kamanda wa polisi wa kanda hiyo maalum ya Tarime na Rorya, Kamishna Msaidizi, Constantine Massawe, alisema jana mjini hapa kuwa bangi hiyo sawa na kilo 4,500 ilikamatwa katika vijiji viwili wilayani Tarime ikiwa imefungwa katika vifurushi maarufu kama vistoni na kuwekwa ndani ya magunia kwa ajili ya kusafirishwa.
Alisema mtuhumiwa wa kwanza aliyekamatwa na kilo 3,000 sawa na tani tatu ni Laurent Wambura (38) ambaye alikamatwa katika kijiji cha Kikomori wakati mtuhumiwa mwingine Marwa Manyinya (25) wa kijiji cha Kiongera alikamatwa na kilo 1,500 sawa na tani 1.5 wakiwa katika maandalizi ya kuisafirisha.
Alisema watuhumiwa hao ambao wote ni wakazi wa kata ya Susuni jirani na mpaka wa
nchi jirani ya Kenya, walikamatwa kufuatia taarifa za siri zilizotolewa na wananchi kwa jeshi la polisi kuhusu kuwapo kwa mpango huo ambapo polisi waliweka mtego uliozaa matunda ya kuwanasa watuhumiwa kabla ya kuvuka mpaka.
“Sisi jeshi la polisi tunaendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanatupatia katika kupambana na vita dhidi ya kilimo cha biashara ya dawa hizi za kulevya lakini nasisitiza kuwa bangi ni kitu kibaya siyo kwa Tarime tu hata kama inasafirishwa na kutumiwa na ndugu zetu jirani,” alisema kamanda Massawe.
Alisema kuanzia sasa jeshi la polisi litawakamata na kuwafikisha mahakamani viongozi wa vijiji ambao ardhi ya maeneo yao wanayoyaongoza yatakutwa yakitumika kwa kilimo hicho.
“Tumeazimia kwamba tutakapopata taarifa kuwa kuna shamba katika eneo fulani wa kwanza kuwakamata ni wenyeviti wa vitongoji na viongozi wa vijiji wakiwemo wataalam wa kilimo kwani haiwezekani mtu akalima bangi hadi hatua ya kuvunwa isifahamike kijijini,” alisema.
Alisema jeshi hilo tayari limetangaza oparesheni ya kufa na kupona kuhusu kudhibiti kilimo na biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yote ya ukanda huo ikiwa ni pamoja na
kuongeza ushirikiano na vyombo vya ulinzi vya nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kurahisisha zoezi hilo.
Aliwaomba wananchi kuendeleza ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za siri ili kuwabaini wote wanahusika na kilimo hicho.
Aliwashauri wananchi kutumia ardhi hiyo yenye rutuba kwaajili ya kulima mazao ya chakula na biashara ikiwemo chai na kahawa badala ya zao la bangi ambalo limekuwa likiwapotezea muda kwa vile imekuwa ikamatwa kabla ya kuuzwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments