Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, amemtumia salamu za pongezi Rais Jakaya Kikwete, Serikali na watanzania wote kuadhjimisha miaka 47 ya Muungano.
Katika salamu zake ambazo nakala yake ilitumwa katika Ubalozi wa Tanzania katika UN, Ban Ki Moon alisema kuwa wakati huu kuliko ilivyokuwa wakati mwingine wowote, dunia inakabiliwa na changamoto nyingi.

Alisema changamoto hizo ambazo zimevaa sura tofauti na uzito tofauti, zinavuka mipaka kutoka taifa moja hadi lingine.
Kiongozi huyo wa UN alisema kwamba kuzitafutia changamoto hizo ufumbuzi kunataka utulivu, umakini, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa .
Alimwelezea Rais Kikwete kwamba, yeye binafsi amedhamiria katika kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa unakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayotokea hivi sasa duniani. Ki Moon alisema UN itahamikisha inasimamia na kutoa matarajio yenye kuridhisha na halisi katika kazi zake tatu kuu za msingi ambazo ni maendeleo, amani na usalama na haki za binadamu.
Alisema kuwa anafarijika na kutiwa moyo na uongozi unaojituma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba anaihesabu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mshirika mkubwa katika kuifanya dunia kuwa endelevu na salama kwa watu wote.