Katika kuonyesha kukerwa na hali ya uhalifu unaozidi siku hadi siku mjini Musoma, wazee wa Kata ya Nyakato, Manispaa ya Musoma, wametaka vijana watakaobainika kujihusisha na uhalifu na ujambazi katika kata hiyo wachinjwe na kuchomwa moto.
Wazee hao wamesema kufanya hicyo itakuwa ni moja ya njia kurejesha amani katika kata hiyo.
Wazee hao kutoka makabila mbalimbali ya Manispaa ya Musoma, walisema hatua hiyo inatokana na kuchoshwa na vitendo vya kihalifu na uvamizi wa mara kwa mara, maarufu ‘mbio za vijiti’ unaofanywa majumbani mwao na baadhi ya vijana katika kata hiyo.
Walisema vitendo hivyo vimewafanya waishi kwa hofu bila amani na wakati mwingine kulazimika kulala nje ya nyumba zao kulinda familia, jambo linalodidimiza ukuaji wa maendeleo katika kata hiyo.
Kauli hiyo ya wazee walitoa juzi mbele ya Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, walipokuwa wakizungumza kwenye kikao cha pamoja cha wazee wa kata hiyo kilichoitishwa na mbunge huyo kwa lengo la kujadili suala la ulinzi na usalama katani humo.
Walisema lipo kundi la vijana katika kata hiyo ya Nyakato Musoma, limekuwa likiendesha ujambazi wa kupora mali za watu, kukata watu mapanga na kuwachinja na kwamba wanapokamatwa na polisi huachiwa huru muda mfupi baada ya kufikishwa kituoni.
Wazee hao wakizungumza kwa jazba mbele ya Mbunge Nyerere ambaye katika kikao hicho alifuatana na Meya wa Musoma, Alex Kisurura pamoja na Diwani wa Viti Maalumu, Miriam Chacha, walisema vijana hao wezi wakikamatwa wachinjwe na kuchomwa moto ili liwe fundisho kwa wengine wenye hulka kama hiyo mbaya.
“Hali ni mbaya sana katika kata yetu hii ya Nyakato, vijana wamekuwa wahalifu wakubwa…dawa yao wakikamatwa wachinjwe tu ili wengine wajue kwamba uhalifu haukubaliki.
Tuliwazaa sisi na kuwalea, lakini leo hii wamekuwa maadui zetu. Hakuna haja ya kuwa na majambazi. Polisi wanapowakamata wanawaachia, sasa dawa yao ni kuwaua kwa kuwachinja,” alisema mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Ogunya kisha kuungwa mkono na wazee wengine.
Katika kikao hicho kilichoanza saa 10:00 jioni na kumalizika saa 12:55 jioni, wazee hao walitumia fursa hiyo kumpongeza mbunge wao Nyerere kwa kuamua kupambana na uhalifu jimboni humo hususani kata hiyo ya Nyakato ambayo inadaiwa uhalifu umeota mizizi miaka mingi.
Aidha, baadhi ya wazee waliwatuhumu wazee wenzao kwa madai kwamba wamekuwa wakiwafadhili na kuwapa baraka vijana wao kwenda kufanya uhalifu na kupora mali za watu na kwamba kuanzia sasa hawapo tayari kulea wahalifu.
“Tuseme ukweli wapo wazee hapa hapa tunafadhili watoto kwenda kuiba mali za watu…tunawafahamu wazee hao, kwa hiyo tumechoka na uhalifu,”alisema Benadetha na kutaka vijana wahalifu na familia zao wapigiwe kura kisha wasulubiwe.
Akizungumza katika kikao hicho cha wazee, mbunge huyo wa Musoma Mjini, Nyerere alieleza kuchukizwa na uhalifu unaofanywa katika kata hiyo ya Nyakato na kwamba uvumilivu umemshinda lazima apambane naokwa mbinu zote.
Alisema anaamini vijana wengi sana walimpigia kura, lakini katika suala la uhalifu, hatawaonea haya bali atapambana nao na kwamba ipo haja ya vijana wahalifu kuanza kupigiwa kura za siri na yeyote atakayepata kura nyingi lazima achukuliwe hatua pamoja na mzazi wake.
“Umefika wakati uvumilivu utanishinda tuanze kushughulikiana tu…siwezi kufumbia macho suala hili la uhalifu, nawaombeni sana wazee wangu tushirikiane kufichua hawa wezi lakini si kwa kuwachinja kwani nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya sheria,”, alisema mbunge huyo.
Alisema atawasiliana na uongozi wa Jeshi la Polisi kuhakikisha wanaondoa kasoro ambazo zimekuwa zikichangia wananchi wengi kujichukulia sheria mkononi.
Katika kikao hicho cha wazee, maazimio mazito manane yalipitishwa, likiwemo la vijana wahalifu wanapokamatwa wachinjwe hadi kufa, uwepo mtandao maalum wa kufuatilia vijana wezi, kufufuliwa kwa ulinzi wa sungusungu na wenyeviti wa mitaa wawe na takwimu za watu wao wakiwemo wahalifu kuwabaini.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments