CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), hatimaye kimetoa siri hadharani ya sababu zilizokifanya kujivua gamba ili kuzaliwa upya kwa lengo la kurejesha imani na umaarufu wake machoni
mwa wanachama wake na wananchi.

Akihutubia maelfu ya wanachama wa chama hicho na wananchi waliojitokeza ili kuilaki
Sekretarieti mpya ya chama hicho katika viwanja vya Bakhresa, Manzese, Dar es Salaam Jumapili, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa alisema zipo sababu sita zilizokifanya chama hicho kujivua gamba.

Alisema matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kote mwaka 2010 yalitoa ishara
kwamba chama hicho kimeanza kupoteza umaarufu wake na wananchi kukosa hatua iliyomfanya Rais Kikwete kuunda Kamati Maalumu ya watu sita, iliyowajumuisha wataalamu
wasio wanaCCM ili kuchunguza kiini cha chama hicho kuanza kupoteza umaarufu na imani
kwa wananchi kwa kasi, Kamati iliyokuwa chini ya Wilson Mukama.

Alisema tathimini ya Kamati ya Mukama, ilieleza sababu kuu sita zilizosababisha wananchi
kuikataa CCM na kuwapigia kura chache mgombea wa urais kupitia chama hicho, Rais Kikwete,
wabunge na madiwani na kukifanya chama hicho kupoteza viti vingi vya ubunge wa majimbo
na wa viti maalumu, hatua iliyofanya ruzuku kupungua.

Alisema Kamati hiyo ilieleza kwamba CCM ilikuwa imebebeshwa mzigo mzito wa kuwa na wanachama wanaoshutumiwa na wananchi kuhusika katika vitendo vya ufisadi na rushwa
na hivyo wananchi kuwaona viongozi wote wa CCM kama ni mafisadi na wala rushwa.

“Hili lilikuwa ni tatizo la kwanza na Mwenyekiti (Rais Kikwete), alichukua hatua kuonesha kuwa sisi si mafisadi wala hatuukumbatii ufisadi na hivyo tumeamua kwa dhati kwamba tutaachana na wanachama wote wenye sifa hizo.”

Kamati ya Mukama pia ilitueleza kwamba kulikuwa na mfumo mbaya wa uendeshaji wa chama hicho, ambapo madaraka kutoka ngazi ya Taifa yalikuwa yakiruka ngazi husika kwa viongozi wa kitaifa kwenda ngazi za chini kutoa maelekezo badala ya kufuata muundo wa Taifa, Mikoa, Wilaya, Kata na Mashina.

“Hili liliwafanya viongozi wetu wa chama kushindwa kuwa karibu na wananchi na hivyo kupoteza ushawishi wa chama chetu machoni mwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

Kamati ilitushauri na sasa tutaanza mara moja kufuata muundo unaokubalika.” Aliitaja sababu ya tatu kuwa ni hali ngumu ya maisha ya Watanzania, ambapo wataalamu walisema chama hicho kimeshindwa kusimamia na kurahisisha maisha ya wananchi na hivyo kushindwa kusimamia kwa vitendo kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.

“Hali ya maisha ipo juu, kuna mfumuko mkubwa wa bei na matatizo makubwa ya kiuchumi.
Wataalamu walisema wananchi sasa wanauliza maisha bora kwa wananchi yapo wapi. Hili
tumelichukua kama changamoto na tunapaswa kulifanyia kazi mara moja.”

Sababu ya nne kwa mujibu wa Msekwa ni kukosekana kwa nguvu za vijana katika ushawishi
na badala yake chama hicho kuwakumbatia zaidi viongozi wazee; ”Walituambia mnayo
hazina kubwa ya vijana lakini hamuwatumii vizuri na tulilichukua hilo na kuanza kulifanyia
utekelezaji mara moja.”

Msekwa aliitaja sababu ya tano kuwa ni kuwepo kwa makundi miongoni mwa wanaCCM, ishara iliyojionesha wazi katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka jana, hatua iliyomfanya Rais Kikwete kuunda Kamati chini ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Msekwa na Abdulrahman Kinana ili kubaini kiini cha makundi hayo.

Sababu ya sita ni CCM kuwapelekea wananchi wagombea wasiokubalika kila uchaguzi unapowadia, hatua aliyosema itafanyiwa kazi ili kutafuta muundo mzuri wa kuwapata wagombea wa CCM wanaokubalika na wananchi. Kwa mujibu wa Msekwa, mbio za urais mwaka 2015, ilikuwa sababu nyingine iliyokuwa inakitia kitanzi chama hicho kutokana na kuibuka kwa watu walioanza kujipanga kwa nafasi hiyo na kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2010/2015.

Alisema sasa CCM inatafuta mfumo mzuri na muafaka wa kumpata mgombea. Alisema kujiuzulu kwa Sekretarieti na Kamati Kuu ya chama hicho ngazi ya taifa ilikuwa ni hatua ya kwanza ya mageuzi ndani ya CCM na kwamba mageuzi hayo yatafuata katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na mashina.

“CCM baada ya kupokea mapendekezo yale ndio maana ikamteua kiongozi wa kamati ile
(Mukama) kuwa Katibu Mkuu wa chama ili kusimamia mabadiliko hayo na kujenga CCM mpya.

Njia kama hii aliwahi kuitumia Mwalimu Nyerere (Julius-Baba wa Taifa), pale tulipokuwa tunaunganisha TANU na ASP ambapo mimi niliteuliwa kusimamia kamati ya kuangalia namna ya kuwa na muundo mzuri wa chama na nilipomaliza akanikabidhi kazi ya Kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa CCM,” alisema Msekwa.

Naye Halima Mlacha anaripoti kutoka Chalinze kwamba CCM haijakosea ‘kujivua gamba’ na kuchagua viongozi wake wapya wa Kamati Kuu na Sekretarieti na kwamba kazi iliyopo mbele yake sasa ni kubadili taswira ya chama hicho iliyochafuka.

Pia viongozi wa chama hicho wapya walioteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa NEC ya chama hicho hivi karibuni, wameendelea kusisitiza kuwa, hawatavumilia wanaokiharibia chama hicho na kutaka suala la ‘kuvua gamba’ lifike ngazi za chini.

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza viongozi hao wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya
CCM, iliyofanyika Chalinze na Kibaha mkoani Pwani, Makamu Mwenyekiti, Bara, Pius Msekwa,
alisema kilichofanyika ndani ya chama hicho ni kubadili taswira mbaya na kuijenga CCM mpya.