JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu 56 wanaodaiwa kuwa ni wahamiaji haramu kwa tuhuma za kuingia nchini pasipo vibali halali vya kusafiria.
Watu hao ambao sita kati yao ni wanawake na wanaume 50 ni raia kutoka nchi za Ethiopia na Somalia na walikutwa wamejificha kwenye msitu wa Kwalaguru ulioko kata ya Kabuku wilayani Handeni.
Ofisa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jaffar Mohamed akizungumza na 'Habarileo' Ijumaa alisema watu hao walikamatwa juzi saa 4.15 asubuhi wakiwa wamejificha katika msitu huo ulioko jirani na Shamba la Mkonge la Kwalaguru.
“Kukamatwa kwa wasafiri hao haramu kumetokana na taarifa za raia wema kwa Polisi waliopo kwenye kituo chetu cha Kabuku ambao waliwajulisha askari kwamba kwenye Msitu wa Kwalaguru ulioko jirani na shamba la mkonge linalomilikiwa na Kampuni ya Kwalaguru Estate kuna watu wengi wamejificha na ndipo harakati za askari kuwakamata zikaendelea," alisema.
Alibainisha kwamba kati ya watu hao 56, raia kutoka nchini Somali ni kumi ambao kati yao yumo mwanamke mmoja huku wahamiaji kutoka Ethiopia waliokamatwa walikuwa 46 wakiwemo wanaume 41 na wanawake watano.
Kwa mujibu wa Kamanda Jaffar watu hao licha ya kukamatwa hapo msituni ni wasafiri wanaotoka Somalia na Ethiopia kwenda Afrika Kusini kwa kupitia nchi za Kenya na Tanzania kwa njia ya barabara.
“Katika mahojiano ya awali alijitokeza mmoja kati yao ambaye tulizungumza naye kwa kutumia lugha ya Kiswahili akichanganya na Kiingereza na ametueleza kuwa baada ya kutoka kwenye nchi zao safari yao imeanzia mjini Nairobi kwa kusafiri na basi dogo ambalo liliwaacha mahali fulani asipopafahamu.
“Kutoka hapo walilazimika kutembea kwa saa moja mpaka mahali pengine ambapo walipanda lori lililowaleta hapo msituni ambapo walikuwa wakiwasubiri waratibu wa safari yao ili wawaunganishe kwenye gari jingine, lakini bila mafanikio na hatimaye wakakamatwa na askari”, alisema Ofisa Upelelezi huyo.
Amebainisha kwamba uchuguzi wa awali wa Polisi umebaini kwamba wasafiri hao haramu wanaosafiri kwa kupitia baadhi ya maeneo ya mkoani hapa wamekuwa wakishushwa njiani na kutakiwa kutembea kwa miguu umbali fulani ili kukwepa ukaguzi kwenye vizuizi vya askari barabarani na kudai kwa tukio hilo walikuwa wakikwepa vizuizi vilivyopo Kabuku na Ntegwe wilayani Handeni.
Hata hivyo, alisema polisi bado wanaendeza mahojiano nao na jana walitarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Handeni kwa tuhuma za Kuingia nchini bila kibali halali.
0 Comments