SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, ameutoa muswada wa sheria ya mapitio ya Katiba kwenye ratiba ya Mkutano wa Tatu wa Bunge unaoendelea Dodoma ili kutoa fursa kwa wananchi kuendele kutoa maoni kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.

Baada ya Makinda kutangaza uamuzi wake bungeni mjini Dodoma, wabunge walishangilia na wengine kupiga vigelegele wakimaanisha kuwa wamefurahia uamuzi huo wa Spika wa Bunge.

Spika amekubali maombi ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba kamati ipewe muda zaidi ili na wananchi wapate muda wa kuufikiria zaidi muswada huo na kutoa maoni yao.

Kamati hiyo hiyo pia imemuomba Spika iandae muswada huo kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi waweze kuusoma wenyewe badala ya kupewa tafsiri tu, na pia ikaomba muswada huo uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi wauelewe na watoe maoni.

Iliomba pia utangulizi wa muswada huo uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe madhumuni ya muswada huo kwa kuwa baadhi yao wanadhani kuwa tayari Bunge limeanza kuandika Katiba.

Makinda amewataka watakaochangia muswada huo wajadili mapendekezo badala ya kulumbana, na pia wanasiasa waache kushindana majukwaani.

“Wanasiasa tuache kushindana majukwaani, tujadili muswada. Maoni, ushauri na mapendekezo ndiyo yatasababisha kutungwa kwa sheria nzuri” amesema Makinda na kuwataka watakaotoa maoni waache malumbano na amewaomba Watanzania kudumisha mila zao za utulivu na amani.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema, muswada huo si mali ya chama chochote cha siasa na kwamba, huu si wakati wa kulaumiana ila kutoa hoja zenye uzito zinazoweza kusaidia kuandika muswada vizuri.

“Nasisitiza utulivu wakati wote wa kazi hii. Kila mwanakamati ajue kwamba shughuli hii inatawaliwa na Kanuni za Bunge na itaratibiwa na kusimamiwa na kamati husika na siyo vyama vya siasa” amesema.

Spika amewaomba wananchi waiamini kamati yake kwa kuwa imejaa watu wenye uzoefu mkubwa na waliobobea katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya sheria.

Makinda amesema, wahusika kwenye vyama vya siasa wanapaswa kutumia busara kutoa mawazo yao na wakisema hili liondolewe wawe pia tayari kusema kiwekwe nini badala yake.

“Waheshimiwa wabunge, kupitia kwenu nawaomba wananchi waepuke uandikaji wa muswada kwa kuleta fujo ya aina yoyote ile” amesema Makinda leo asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Spika wa Bunge ameitaka Serikali iuwasilishe muswada huo kwa lugha ya Kiswahili na uandikwe kwenye magazeti mbalimbali ili wananchi wausome, waulize maswali na waondoe jazba ambazo hazina mantiki.

“Muswada kwa hatua tuliyofikia si wakati wa kulaumu au kulaumiana bali ni kutoa hoja zenye uzito zinazoweza kusaidia muswada mzuri” amesema na kusisitiza kwamba, uandikaji wa Katiba mpya ya nchi uwe chanzo cha kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha utaifa wetu kwa kuwa lengo letu ni ni kuwa na Tanzania moja yenye amani na utulivu.

“Aidha ninaiagiza kamati iniletee ratiba na utaratibu wa kukamilisha kazi hii ili muswada huu uweze kusomwa mara ya pili katika mkutano ujao wa Bunge” amesema Makinda na kuwaomba wananchi watoe maoni yao kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kupitia Ofisi za Bunge zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, na Zanzibar.