Washukiwa wengine watatu miongoni mwa wale sita wanaoshukiwa kwa kupanga na kutekeleza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya wanafika mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC mjini The Hague Ijumaa alasiri.
Naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa watakaopanda kizimbani Ijumaa, kuipa mahakama fursa ya kuthibitisha utambulisho wao, kuhakikisha wanafahamu uhalifu wanaodaiwa kuutekeleza, na kuwaelezea haki zao kama washukiwa.
Wengine ni mkuu wa utumishi wa Umma ambaye pia ni katibu wa baraza la mawaziri Francis Muthaura, na aliyekuwa mkuu wa jeshi la Polisi nchini Kenya Hussein Ali.
Mahakama ya ICC inamlaumu Bwana Kenyatta na Bwana Muthaura kwa kupanga na kufadhili mauaji, ubakaji na kuhamisha watu kwa lazima katika maeneo ya Naivasha na Nakuru.
Jenerali Hussein Ali ambaye alikuwa mkuu wa Polisi analaumiwa kwa kukosa kuzuia makundi ya vijana wanaodaiwa kutekeleza uhalifu huo.
Siku ya Jumatano washukiwa wengine watatu walifika mbele ya mahakama hiyo.
Baada ya kikao hicho mmoja wa washukiwa, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto , aliwaambia waandishi wa habari kwamba ana hakika ataondokana na masaibu haya.
‘’Tutapata sasa nafasi ya kujibu uvumi na uongo ambao umeletwa katika mahakama hii , na tuko tayari kwa sababu ukweli ukidhihiri uongo utajitenga’’ , alisema Ruto.
Wengine waliofika mahakamani Jumatano ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic (ODM) Henry Kosgey na mtangazaji wa redio ya kijamii Joshua Arap Sang.
Jaji kiongozi katika kesi hiyo Ekaterina Trendafilova alitangaza kwamba siku ya kuthibitishwa kwa mashtaka ya washukiwa itakuwa Septemba tarehe moja mwaka huu.
Vile vile Bi Trendafilova alimwagiza kiongozi wa mashtaka Luis Moreno Ocampo kutangaza wazi ushahidi alionao dhidi ya washukiwa katika kikao kitakachofanyika tarehe 18 mwezi huu, kwenye mahakama ya ICC.
Hii itatoa nafasi kwa washukiwa na mawakili wao kuanza kuandaa utetezi.
Zaidi ya watu 1,200 waliuwawa kwenye ghasia hizo za Kenya, zilizosababishwa na ubishi kuhusu matokeo ya kura ya Urais.
Kinachodhihirika kuhusu washukiwa wanaofika mbele ya mahakama Ijumaa ni uwakilishi wa mawakili mashuhuri duniani.
Bwana Kenyatta anawakilishwa na mawakili watatu kutoka Uingereza wakiwemo Steven Kay na Gillian Higgins, ambao walikuwa watetezi katika kesi iliyomkabili Rais wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic.
Wakili mwingine katika jopo la Bwana Kenyatta ni Benjamin Joyes.
Bwana Muthaura anawakilishwa na miongoni mwa wengine Karim Ahmed Khan, ambaye amekuwa mshauri katika mahakama zinazoshughulikia jinai za Yugoslavia na Rwanda.
Wengine katika jopo la kumwakilisha Mkuu huyo wa utumishi wa umma ni Kennedy Ogeto na Muriuki Mugambi.
Generali Hussein Ali anawakilishwa na miongoni mwa wengine Gregory Kehoe, ambaye alikuwa mshauri wa mahakama iliyomshtaki rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.
Wengine ni Evans Monari na Gersham Otachi.
Bwana William Ruto pia anawakilishwa na pamoja na wengine mwanasheria mashuhuri kutoka Uingereza David Hooper, ambaye pia katika kesi nyingine anamwakilisha Germain Katanga, mmoja wa washukiwa wa uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wengine katika jopo lake ni Kioko Kilukumi, Kigen Katwa na Kithure Kindiki.
Bwana Henry Kosgey anawakilishwa na mwanawe Allan Kosgey, George Oraro na Julius Kemboi.
Mawakili wa Bwana Joshua Arap Sang ni ni Katwa Kigen, Joel Kimutai Bosek na Philemon Koech.
Wakati wa kikao cha kutangaza wazi ushahidi dhidi ya washukiwa tarehe 18 mwezi huu, kiongozi wa mashtaka Luis Moreno Ocampo atatakiwa kueleza idadi ya mashahidi na idadi ya taarifa za maandishi atakazotumia.(source bbc)
0 Comments