WATOTO wanne wa Shule ya awali ya Nia iliyopo Kimara B Matosa, wilayani Kinondoni wamekufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa jirani na shule hiyo wakati wakichezea bembea.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 6.30 mchana katika shule hiyo inayomilikiwa na Jacqueline Sarungi (42), mkazi wa Kimara B Matosa.

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, siku hiyo watoto hao walipokuwa wakibembea, ghafla waliangukiwa na ukuta wa nyumba inayomilikiwa na Amani Mashika jirani na shule hiyo na watoto hao kufa papo hapo.

Aliwataja watoto hao kuwa ni Gladness Shimwela (5), Devota Living (5), Ludacris Lawrence (3) na Isaack Ndosi (5) wote wa Kimara B Matosa.

Waliojeruhiwa ni Angela Jonas (5), Asumbwene Uswege (5) na Lilian Dominic (7), wa eneo hilo pia na ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi.

Miili ya watoto hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi, Kimara na upelelezi wa tukio hilo ili kujua chanzo chake unaendelea.

Wakati huo huo, mtoto mwingine kichanga, amekufa baada ya kudaiwa kutumbukizwa chooni na mama yake, muda mfupi baada ya kuzaliwa akiwa hai.

Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela, mtoto huyo wa kiume alizaliwa chooni na baada ya hapo mama yake alimsukumiza kwenye tundu la choo huku shangazi yake, Shadya Ally (18) akishuhudia.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kenyela alisema Shadya aliiambia Polisi kuwa wifi yake mkazi wa Mikocheni, Happy Freddy (28), alifanya hivyo saa 4 usiku baada ya kutoa taarifa kuwa alikuwa akijisikia uchungu.

Kwa mujibu wa Kamanda, Shadya alisema katika taarifa yake Polisi kuwa baada ya wifi yake kujisikia uchungu, alimwomba (Shadya) amsindikize hospitalini na wakatoka kwenda hospitali.

“Wakiwa njiani karibu na Kanisa la Walokole, Happy aliomba kuingia choo cha jirani ili ajisaidie na Shadya kumsubiri nje, lakini ghafla alisikia sauti ya mtoto kutoka chooni na wifi yake akiwa humo,” alisimulia Kamanda Kenyela.

Kutokana na hali hiyo, inadaiwa Shadya alimfuata wifi yake na kukuta kichanga hicho kikiwa pembeni mwa tundu la choo na wakati akimulika vizuri kwa simu yake ya mkononi, ghafla wifi alimsukumia shimoni mtoto kwa mguu huku akidai ameharibika.

Mwili wa mtoto huyo uliopolewa na wananchi wa eneo hilo kwa kushirikiana na polisi na umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala huku polisi wakiendelea na upelelezi huku wakimshikilia mtuhumiwa.