Walisema hayo katika kongamano la kujadili Madaraka ya Rais katika katiba ya Tanzania na Zanzibar, iliyowasilishwa na mwanaharakati, Salma Maulid, lililofanyika mjini Zanzibar.
Mwanasiasa mashuhuri Zanzibar, Mohammed Yussuf, alisema Rais wa Zanzibar na wa Muungano wamepewa madaraka makubwa katika uteuzi wa viongozi na ndio maana wakati mwingine wanateua watu wasiokuwa na uwezo.
Alisema ni vizuri kuwepo na mfumo kama wa Marekani kwa nafasi za uongozi, ambapo kabla ya mtu kuteuliwa huchunguzwa na taasisi maalum, ili kujua uwezo na uadilifu wake kabla ya kutangazwa kushika wadhifa huo.
Akichangia katika mada hiyo, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Ali Ali Hassan, alisema kuna haja kofia ya Rais itenganishwe ili watu wajue ni wakati gani anakuwa Rais na wakati gani kiongozi wa chama chake cha siasa.
Alisema mfumo unaotumika hivi sasa kwa Rais upande mmoja na upande mwengine ni kiongozi wa chama chake unakwaza demokrasia na kuwanyima watu nafasi ya kumkosoa katika uwanja wa kisiasa.
Alisema suala la uteuzi wa nafasi za viongozi Zanzibar lina kasoro kwa vile hufanyika uteuzi bila ya kuangaliwa vigezo, sifa na kutokuwepo uwazi na wakati mwengine hata usaili unakuwa haufanyiki.
Alieleza kwamba kuna watu wanateuliwa kwa sababu wapo karibu na wahusika na hawaangaliwi sifa zao na uwezo wa kazi, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa na kuwekewa msingi mzuri wa kisheria.
Aliongeza kwamba Katiba ya Zanzibar imempa uwezo mkubwa Rais wa Zanzibar, kwa vile anaweza akakataa kusaini muswada wa sheria uliokwishapitishwa na Baraza la Wawakilishi, mbali na uwezo wa kuliuvunja baraza hilo.
Alitoa mfano kuna sheria zilizopitishwa wakati wa utawala wa awamu ya tano, chini ya Rais Dk. Salmin Amour lakini hakuzisaini hadi alipoingia madarakani Rais wa awamu ya sita, Abeid Amani Karume.
Naye Salma Kombo akichangia mada hiyo alisema maliasili za serikali ikiwemo ardhi imefika wakati katiba ikafanyiwa marekebisho na kusimamiwa na Baraza la Wawakilishi au Bunge, ili kuepusha matumizi mabaya yanayoafanywa na viongozi.
Alisema Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na matumizi mabaya ya ardhi na majengo ya serikali kwa viongozi na kutaka jambo hilo liwekewe msingi mzuri, ili wananchi wanufaike nazo badala ya watu wachache.
Salma alisema baadhi ya viongozi Zanzibar wametumia mali za umma kwa maslahi binafsi, ikiwemo kujigawia maeneo ya ardhi na majumba ya serikali, huku baadhi ya watu na viongozi waliostaafu wakinyang’anywa mali hizo na wengine kuachiwa.
Alipokuwa akiwasilisha mada hiyo, Salma Maulid, alisema katiba ya Zanzibar imempa mamlaka makubwa Rais kama vile kutoa msamaha kwa mtu yoyote aliyehukumiwa na mahakama, uwezo wa kuahirisha uchaguzi mkuu pamoja na kuwa na haki ya kukataa ushauri.
Alisema uwezo huo wa Rais unajidhihirisha hata katika baraza la mawaziri la sasa, ambapo kuna mawaziri wasiokuwa na Wizara maalum, wakati Zanzibar ina idadi ndogo ya wananchi na uchumi mdogo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar, Is-hak Ismail Sharif, alisema Zanzibar imeelekea kujenga kikundi kisichoguswa na sheria kitendo ambacho ni kinyume na misingi ya haki za binaadamu.
Alieleza kwamba kuna watu wanafanya makosa ikiwemo kusababisha ajali na vifo barabarani, lakini hawachukuliwi hatua kitendo ambacho ni kinyume na misingi ya utawala bora.
Alitoa mfano askari wa jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hivi karibuni walipiga raia kutokana na mtu mmoja anayesadikiwa mke wa askari mmoja kuibiwa, na hakuna hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa, licha ya watu kadhaa kupigwa hadi kulazwa hospitali.
Mjadala wa huo ni mwendelezo wa matayarisho ya mchakato wa wananchi kutoa maoni juu ya katiba mpya unaotarajiwa kufanyika hapo baadaye.
0 Comments