MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, imetoa zuio la muda dhidi ya Askofu Mathayo Kasagara wa Dayosisi ya Ziwa Rukwa kuingia eneo la Kanisa la Watakatifu Wote mjini hapa ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kutokea kanisani hapo.

Zuio hilo lilitolewa Mei 13 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Manase Goroba, baada ya maombi ya dharura yaliyowasilishwa na Wakili wa waombaji, Ileth Mawalla kutoka Kampuni ya Mawakili ya S. Mawalla Law Consultancy & Attorneys ya hapa.


Walalamikaji hao ambao ni waumini zaidi 400 wa Kanisa la Watakatifu Wote la Anglikana, wanapinga uchaguzi wa Askofu Kasagara uliofanyika mwaka jana kuiongoza dayosisi hiyo.


Katika shauri hilo, waumini wa Kanisa hilo wanawakilishwa na wenzao wawili, Fulgence Rusunzua na Rojas Bendera, baada ya kukubali maombi ya kuwakilishwa katika shauri la msingi namba 11/2011 ambapo waumini 193 wamejiorodhesha.


Hakimu Goroba kupitia hati ya dharura iliyotolewa mahakamani hapo na kusikilizwa, alitoa amri ya zuio la muda dhidi ya Askofu Kasagara la kuingia na kukaribia eneo hilo la Kanisa hilo ili kuepusha uvunjifu wa amani hadi shauri la msingi litakapotolewa uamuzi.


Katika shauri lao la msingi, waumini hao wanapinga tamko la Kamati ya Maofisa wa Kanisa Anglikama Tanzania kuhusu mgogoro wa Dayosisi ya Ziwa Rukwa, lililosainiwa na Askofu Mkuu, Valentino Mokiwa na Katibu Mkuu, Dk. Dickson Chilongani, ambalo linawataka waumini hao kumtambua Askofu Kasagara kuwa Kiongozi wao halali wa kiroho.


Pia tamko hilo la Kamati ya Maofisa wa Kanisa Anglikana Tanzania, linawataka waumini wa Kanisa hilo kukabidhi mali yote ya Kanisa kwa Dayosisi ya Ziwa Rukwa inayoongozwa na Askofu Kasagara, kinyume na matarajio, kuwa mgogoro huo ungemalizwa kwa amani na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa niaba ya Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa hilo.


Kwa hali ilivyo, waumini wa Kanisa hilo ambao ni zaidi ya 400 hawakubaliani na tamko hilo

ambalo Serikali ya Mkoa wa Rukwa bila uchunguzi wa kutosha, iliiandikia Kamati inayoongoza Kanisa hilo ikiamini kuwa ni kundi la watu wachache, kinyume na hali halisi, ikiwataka wakubaliane na tamko hilo.

Mawalla akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, alisema kwa kuwa shauri liko mahakamani hapana budi kuiachia Mahakama ifanye kazi zake kwa uhuru.(source Habari leo)