Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (GNU) imeanza kupata mafanikio katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya visiwani humu.
Maalim Seif alisema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini wa Chama Cha Wananchi (CUF), katika ukumbi wa Jamatkhan, mjini hapa.
Alisema vijiwe vya watumiaji wa dawa za kulevya na wauzaji, sasa vimedhibitiwa na vyombo vya dola tangu kukabidhiwa dhamana ya kupambana na biashara hiyo haramu katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Aliyataja maeneo ambayo yamedhibitiwa kuwa ni Mkele na Kwaalinatu, kufuatia operesheni mbali mbali na mpango shirikishi wa wananchi kuwafichuwa wauzaji wa dawa hizo katika mitaa yao.
Hata hivyo, alisema bado kuna vichaka vya wauza unga katika Mji Mkongwe wa Zanzibar na kuahidi Serikali itahakikisha inasafisha kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo hayo.
Alisisitiza kuwa tatizo la biashara ya dawa za kulevya litadhibitiwa Zanzibar iwapo wananchi watatoa ushirikiano ya kutosha kwa Serikali kupitia mpango wa Polisi Jamii.
Maalim Seif alisema matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa yakiathiri vijana wengi wakati ndio nguvu kazi ya taifa na ndio maana Serikali ya Zanzibar awamu ya Saba imeamua kuongeza nguvu za ziada katika kupambana na tatizo hilo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments