Maafisa 8 wakuu waliojitenga na jeshi la Kanali Muammar Gaddafi, wametoa wito kwa wanajeshi wenzao kuwaunga mkono na kuwasaidia waasi.
Mmoja wa wanane hao alishutumu vikosi vya Gaddafi kwa kutekeleza "mauaji ya halaiki".


Wanaume hao wanaosemekena kujumuisha majemedari watano walihutubia waandishi wa habari mjini Rome, Italia.

Wakati huo huo Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amefanya mashauriano na Kanali Gaddafi, mjini Tripoli, katika juhudi za kuleta suluhu kwa mzozo huo unaoendelea.
Mmoja wa majemedari hao waliozungumza na waandishi wa habari mjini Rome na anajulikana kama Oun Ali Oun, alisoma ujumbe wa wito kwa wanajeshi wenzake na maafisa wa usalama kujitenga na utawala huo.
Pia alikanusha "mauaji ya halaiki " na "mashambulio dhidi ya wanawake katika miji tofauti ya Libya"
Jemedari mwengine, Melud Massoud Halasa, aliambia waandishi wa habari kwamba vikosi vya Kanali Gaddafi "vimebaki na 20% tu ya uwezo" tofauti na walivyokuwa kabla ya mapigano, na "majemedari wanaomuunga mkono si zaidi ya 10".
Waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa Libya, Abdel Rahman Shalgam,ambaye sasa anaunga mkono waasi na alikuwepo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari amesema katika siku za hivi karibuni,wanajeshi 120 wamehamia upande wa upinzani.
Tangu kuanza kwa makabiliano mwezi Februari maafisa wa jeshi,mawaziri wa serikali, na mabalozi wamemkimbia Kanali Gaddafi.