KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, akifafanua jambo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichowaandalia Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. Kulia ni Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba. (Na Mpigapicha Wetu).

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amesema kinachofanyika sasa katika chama hicho ni mageuzi makubwa ya kukisafisha na kwamba si ajali.

Mukama amesisitiza kwamba, CCM itaendelea kupambana na ufisadi.


Amebeza kauli za baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitakufa, akisema “Chadema itakufa mara mia, CCM itabaki.”


Mukama amewaambia watendaji na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam kuwa ilichofanya hivi karibuni CCM ni mabadiliko yenye utashi na si ajali, kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ya haja ya kuwapo kwa mageuzi katika chama hicho tawala.


“Kilichofanyika ni kwa utashi, siyo ajali. Ulifanyika uchambuzi uliojengwa katika misingi ya kukifanya chama kiendelee kuongoza,” alisema Mukama jana katika mkutano wake huo wa kwanza mkubwa na vyombo vya habari tangu ashike wadhifa huo mapema Aprili.


Alisema, vikao vya chama hicho havikukurupuka kufanya maamuzi ikiwemo kujiuzulu kwa Kamati Kuu na Sekretarieti, bali vilifanya hivyo kwa nia ya kuruhusu mageuzi hayo ambayo alisema maamuzi magumu zaidi yatarajiwe kuelekea mageuzi hayo.


“Tuko kwa utashi, msingi wa mabadiliko ni lazima uwe ndani ya chama chenyewe. Na mageuzi haya yana lengo la kukisafisha chama, siyo kukiua,” alifafanua kada huyo wa miaka mingi katika CCM.


Alisema, kama kuna watu wanatilia shaka mageuzi hayo yaliyoendana na dhana ya kujivua gamba, wasubiri waone nini kitafanywa na chama hicho, kwa sababu kina dhamira ya dhati ya mageuzi hayo.


“Tuacheni, tupeni nafasi, subirini….kweli hili hatutafanya ajizi, alieleza Mukama na kuongeza:


“CCM imejivua gamba kwa kujaza safu upya za uongozi wake ndani ya Kamati Kuu na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Hii ni hatua ya mwanzo katika mchakato wa mageuzi makubwa ndani ya chama.”


Alisema, lengo la hatua hiyo ya mwanzo ni kupata viongozi wenye mtazamano, msimamo na vitendo vinavyooana na mwelekeo wa mageuzi yanayotarajiwa kufanywa na CCM.


“Ni kwa sababu hiyo CCM katika mchakato wake wa kufanya mageuzi makubwa imeanza na suala la aina ya viongozi wa kufanikisha mchakato huo,” alieleza.


Mbali na Mukama, Sekretarieti mpya inaundwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Vuai Ali, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu wa Oganaizesheni na Mipango Asha Abdallah Juma na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, January Makamba.


Nape, Nchemba na Makamba walihudhuria katika mkutano huo wa jana na wanahabari ambao Mukama alisema ni muhimu kwa sababu CCM kama taasisi ya kisiasa na taasisi za vyombo vya habari, wote wana nafasi muhimu katika ujenzi wa mustakabali wa nchi.


Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi, Mukama alisema, Chama Cha Mapinduzi kitaendeleza mapambano dhidi ya tatizo hilo na kwamba itachukua hatua stahili kwa wanachama wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwa kufuata taratibu za maadili za chama hicho.


“Tutaendeleza mapambano dhidi ya ufisadi, na hilo limeelezwa vyema katika azimio letu la 15 la NEC mjini Dodoma, likiwataka wanachama wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wapime na wachukue hatua dhidi ya tuhuma hizo.


“Lakini pia Mwenyekiti wa Taifa katika kufunga mkutano wa NEC alieleza kuwa chama hakitakuwa na ajizi katika kupambana na ufisadi na kuwataka wanachama hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wapime na wachukue hatua wenyewe, lakini kama hawatafanya hivyo, chama kitawawajibisha,” alieleza Mukama.


Alifafanua zaidi suala hilo la ufisadi kwa baadhi ya wanachama wao baada ya kuulizwa kuwa haoni kwa nini watuhumiwa wasipelekwe kwenye vyombo kama Takukuru, alisema wanachofanya wanachama hao ni kuwajibika kisiasa kama taratibu za chama zilivyo.


Aidha, alisema kwa rekodi zilizopo hakuna mahali ambako CCM ilieleza kuwa watuhumiwa hao wa ufisadi wamepewa siku 90 wajipime wenyewe, kama chama hicho hakifanya maamuzi juu yao.


“Hizi siku 90 sijui zimetoka wapi…rekodi ni hizo nilizowasomea (azimio la 15 na hotuba ya Mwenyekiti ya kufunga kikao cha NEC). Na kawaida NEC inakutana baada ya miezi minne, sasa siku 90 za wapi,” Alihoji Mukama.


Akijibu hoja kuwa CCM inakufa, Mukama alisema chama hicho ni taasisi iliyojengwa kwa misingi imara na yenye utajiri na rasilimali, hivyo haoni kifo chake.


“Chadema itakufa mara mia, lakini CCM haiwezi kufa, imejengwa kwa misingi imara,” alieleza Mukama.


Kwa upande wake, Nape alisisitiza kuwa usafi wa wanachama wa chama hicho hauwezi kupangiwa na mtu na kusisitiza kuwa “CCM ni taasisi kubwa. Chadema ni fotokopi tu.”