RAIS Jakaya Kikwete amesema, ingawa mauaji ya kiongozi wa Mtandao wa kigaidi wa Al- Qaeda, Osama bin Laden si jambo la kufurahia, lakini yametoa ahueni katika vita dhidi ya ugaidi.
“Huwezi kufurahia kifo cha mtu kwa kuwa tumefundishwa kupenda hata maadui zetu, lakini naweza kusema kutakuwa na ahueni,” alisema Rais Kikwete.
Akijibu swali juu ya mauaji hayo katika mkutano wa waandishi wa habari uliohusu maazimio ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Habari na Uwajibikaji wa Afya ya Wanawake na Watoto, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisisitiza kuwa alitarajia Osama akamatwe na kushitakiwa ili haki itendeke.
“Mtu aliyekuwa akitafutwa ili ashitakiwe nimeambiwa hayupo tena ndiyo hivyo,” alisema Rais Kikwete.
Alikumbushia kuwa Agosti 7, 1998 Ubalozi wa Marekani nchini ulilipuliwa na Watanzania 11 wakauawa na siku hiyo hiyo karibu muda sawa, Ubalozi wa Marekani nchini Kenya nao ulilipuliwa.
Kutokana na milipuko hiyo, Tanzania ilianzisha uchunguzi ambao Rais Kikwete alisema baadhi ya watu walihisiwa kuhusika, lakini mshukiwa mkuu alikuwa Osama.
Katika uchunguzi huo kwa mujibu wa Rais Kikwete, mmoja wa watuhumiwa ambaye ni Mtanzania, alikamatwa nchini Pakistani na kufungwa katika Gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba.
Baadaye Mtanzania huyo, Mohamed Ghailani, alifikishwa mahakamani nchini Marekani ambako Rais Kikwete alisema haki ilitendeka.
Jumatatu , Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kifo cha Osama, ikiwa ni takribani miaka 10 baada ya shambulizi la ugaidi lilitokea Septemba 11, mwaka huu Marekani na kuua zaidi ya watu 3,000.
Kutokana na taarifa hiyo ya kushtukiza viongozi mbalimbali duniani wamempongeza Obama kwa ushindi na kifo cha kiongozi huyo na kuuita ushindi huo kuwa ni wa kihistoria.
Katika hotuba yake aliyoitoa juzi usiku, Obama alisema katika operesheni iliyofanywa na Marekani wamemuua kiongozi huyo wa al-Qeda nchini Pakistan na kuuweka mwili wake chini ya ulinzi.
Mapema Jumapili Marekani ilizindua operesheni yake dhidi katika eneo la Abbottabad nje ya mji mkuu wa Pakistan, Islamabad na baadaye kuthibitisha kuwa Osama ni mmoja kati ya magaidi waliokufa katika mapigano hayo, alisema Obama.
Vyanzo vya habari vya Pakistan vimethibitisha kutokea kwa kifo hicho cha Osama, hali ambayo Obama ameiita ni moja kati ya mafanikio makubwa ya Marekani na kwamba muda mfupi baada ya kuwa Rais mwaka 2009, alimtaka Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi nchini humo kuweka suala la kukamatwa ama kuuawa kwa Osama kipaumbele.
Alisema Marekani ilipata taarifa za kumfuatilia Osama tangu Agosti mwaka jana na kufanya tathmini ambapo walibaini kuwa alikuwa amejificha ndani ya Pakistan na kwamba kwa kushirikiana na Pakistan wamemuua kiongozi huyo pamoja na mtoto wake wa kiume, mwanamke mmoja na wafuasi wake watatu.
Aidha, katika operesheni hiyo iliyohusisha helikopta nne na kuchukua takribani saa mbili, watu 12 wakiwemo watoto sita, wanawake wake wa Osama wawili na marafiki zake wanne wa karibu wamekamatwa.
Osama ambaye alizaliwa nchini Saudi Arabia mwaka 1957, amekuwa akifahamika kama kiongozi wa kundi la ugaidi duniani kote na kuhusishwa na matukio mbalimbali ya mashambulizi nchini Marekani likiwamo la Septemba 11, 2001.
Kwa mujibu wa Ofisa Mwandamizi wa Marekani mwili wa Osama umezikwa baharini kwa kufuata sheria na taratibu zote za Kiislamu.
“Hili ni jambo tunalolipa kipaumbele na ndio maana tumefuata taratibu zote,” alisema.
Muda mfupi baada ya kutangazwa kifo cha Osama, Msemaji wa kundi la Taliban nchini Pakistan lilikanusha taarifa hizo na kudai kuwa bado Osama yuko hai.
0 Comments