Urasimu umetanda katika uchunguzi wa sampuli za mabaki ya ‘egg chop’ zilizodaiwa kuwa na sumu, ambazo ziliua watu wawili jijini Dar es Salaam baada ya kuzila.
Uchunguzi huo ulihusisha Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Kwa takribani zaidi ya miezi miwili sasa uchunguzi huo umekuwa ukifanyika, lakini NIPASHE lilipowatafuta wahusika kutoa majibu ya wamekuwa wanapiga chenga.
TFDA ilipoulizwa mara kadhaa ilisema kwamba wasemaji wa suala hilo wamesafiri kwenda mikoani, huku Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikidai kwamba haijui chochote.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limedai kwamba awali uchunguzi huo ulikwama kutokana na kusubiri majibu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo, hadi jana polisi imeshindwa kuweka bayana uchunguzi wa sakata hilo ili umma ujue kilichotokea na kusababisha vifo.
Tukio hilo lilitokea mapema mwaka huu katika duka la kuuzia mikate la Royal Oven Bakery lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kutokea tukio hilo, zaidi ya sampuli 15 ya mabaki ya chakula pamoja na sehemu ya miili ya waliokufa vilifanyiwa uchunguzi.
Katika tukio hilo watu waliokufa ni Kharafa Shaban na mtoto wake Faidha Shaban (4), wakati wengine saba walijitokeza kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa nao walipatwa na tatizo la kuharisha na kutapika baada ya kula chakula hicho.
0 Comments