Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema atakata rufani kwa CCM ngazi ya Taifa kupinga adhabu aliyopewa na chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam ya kutogombea nafasi yoyote ya uongozi wa chama kwa miezi 18.
Azzan amesema adhabu aliyopewa ni ya uonevu na hakutendewa haki kwa sababu aliowatuhumu ndio waliokaa na kumpa adhabu hiyo.
Azzan aliitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam kujivua gamba kwa sababu baadhi ya wajumbe wake wanajihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi na kwamba walimhujumu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Baada ya kuwatuhumu, viongozi hao katikati ya wiki hii walimpiga kufuli la kumzuia kueleza tuhuma hizo kwa umma na kumtaka awasilishe kwenye vikao rasmi vya chama.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Azzan alisema anakusudia kuwasilisha rufaa yake makao makuu ya chama wiki ijayo ili apate haki yake.
“Nitaiwasilisha rufaa hiyo makao makuu ya chama wiki ijayo…nalazimika kueleza hadharani nia yangu hii kwa sababu hata hao walionikataza nisiongee kwenye vyombo vya habari walitumia njia hiyo hiyo kuutangazia umma,” alisema.
Alisema anashangaa kupewa adhabu huku watuhumiwa wakishindwa kujibu hoja za tuhuma alizotoa dhidi yao. “Hao niliowatuhumu wamekuwa waendesha mashtaka na mahakimu,” alisema.
Azzan alisema kamati hiyo ya siasa haikumtendea haki na hata walipomuita kwa ajili ya kumhoji tuhuma alizozitoa, alishangaa kuonewa huku wengine wakimshambulia kama mtoto mdogo, jambo ambalo halikumpa uhuru wa kujielezea.
Alisema kilichofanyika katika kikao hicho ni kumshambulia badala la kujibu tuhuma alizozitoa.
Hata hivyo, Azzan alisema aliamua kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na tuhuma hizo baada ya kuona kamati hiyo ya siasa haikuwa na wazo la kufanya kikao kwa mujibu wa sheria.
“Nilikuwa nasubiri kwa hamu kikao hicho kiitishwe baada ya uchaguzi kumalizika ila matokeo yake kamati hiyo imekaa kimya na ndio maana nimeamua kulizungumzia katika vyombo vya habari,” alisema na kuongeza: “Wanadhani ningelizungumzia wapi wakati walikuwa hawana hata mpango wa kuitisha kikao.”
Alisema alipatiwa barua za kukatazwa kutoendelea kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya habari, lakini alishangazwa kuona kamati hiyo ikizungumza na waandishi wa habari.
Azzan alithibitisha kupokea barua ya karipio juzi jioni na kusema kuwa msimamo wake utabaki pale pale kuwa sekretarieti ya mkoa inatakiwa ijiuzulu ili uchaguzi ujao waweze kurudisha majimbo yao yaliyochukuliwa na upinzani.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema kuwa suala hilo hataweza kulizungumzia kutokana na kwamba halijawafikia.
“Ni mapema sana mimi kuzungumzia sakata hilo kwani halijatufikia na tukifanya hivyo tutakuwa tumeingilia ngazi za chini yaani Sekretarieti ya Mkoa,” alisema Nape alipozungumza na NIPASHE kwea njia ya simu jana.
Hata hivyo, alisema suala hilo halihusiani moja kwa moja na idara yake na kwamba hayo ni masuala ya kiutawala.
Nnauye alisema milango ya makao makuu ya chama iko wazi kupokea malalamiko ya upande wowote ambao utaona haukutendewa haki.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments