HUDUMA ya tiba inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwaisapile, juzi ilichelewa kuanza kwa saa kadhaa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa waliofika kupata kikombe cha Babu baada ya vurugu kuzuka.
Vurugu hiyo ilizuka ghafla baada ya mlinzi wa Mchungaji Mwaisapile, Fred Nsajile kupambana na mwandishi wa habari wa Channel Ten, Jamila Omar akimfukuza kupiga picha eneo la Mchungaji huyo.
Tukio hilo, ambalo lilikusanya umati, lilitokea muda mfupi baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa Mtandao wa Vodacom uliofanyika katika Kijiji cha Samunge na makabidhiano ya simu aliyopewa Mchungaji Mwaisapile na maofisa wa Vodacom akiwa nyumbani kwake.
Mlinzi huyo wa Mchungaji ambaye ndiye Msaidizi wake, katika harakati za kumuondoa kwa nguvu mwandishi huyo, alidaiwa kuharibu kamera ya kituo cha Channel Ten na kusababisha suala hilo kufikishwa Kituo cha Polisi Loliondo.
Kabla ya vurugu hizo, mlinzi huyo wa Mchungaji Mwaisapile, alimzuia mwandishi huyo kushuhudia makabidhiano ya simu aliyopewa Mchungaji huyo, lakini Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliyekuwa mgeni rasmi aliagiza mwandishi huyo kuruhusiwa kufanyakazi yake kwa mujibu wa taratibu.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kukamilika makabidhiano hayo na Mkuu huyo wa Wilaya kuondoka, ndipo mlinzi huyo wa Mwaisapile alianza kumfukuza tena mwandishi huyo eneo hilo jambo lililozua tafrani.
"Kazi ya Vodacom iliyokuleta imekwisha ondoka hapa kwa Mchungaji, ondoka ondoka," alisikika akipaza sauti mlinzi huyo ambaye alifikia hatua ya kukunja blauzi ya mwandishi huyo na kumchania sidiria.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Samunge, Jackson Sandea, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Michael Lengume na baadhi ya polisi ndio walifanikiwa kuzima vurugu hizo baada ya kumzuia mlinzi huyo asiendelee kupambana na mwandishi huyo.
"Tafadhali Fred mwache huyu dada mbona hakuna tatizo hapa,"alisikika akisema Diwani wa Samunge akimuasa Nsajile.
Kutokana na tukio na matukio mengine ya vurugu baina ya mlinzi huyo wa Mchungaji na wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Samunge, Lengume amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani kuweka utaratibu wa kukaa kwa zamu walinzi wa Mchungaji huyo.
"Kwanza sisi kama Serikali ya Kijiji hatujawahi kuomba ulinzi kama huu, sasa hivi hata sisi viongozi kuonana na Mchungaji ni tatizo, watu wanapigwa ovyo na inaonekana kama kijiji kimevamiwa," alisema Lengume.
Kuondolewa kwa mwandishi huyo, kunatokana na utaratibu wa kuzuia waandishi kwenda kuonana na Mchungaji Mwaisapile bila kuwa na kibali toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, utaratibu ambao umekuwa ukilalamikiwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Tukio hilo la wanahabari kutoelewana na Nsajile si la kwanza, kwani mwandishi mwandamizi wa mwananchi, Nevile Meena pia nusura apate kipigo kutoka kwa ofisa huyo sambamba na mpigapicha Emanuel Helman na wanahabari kadhaa wa ndani na nje ya nchi ambao baadhi yao walivunjiwa kamera.
Hata hivyo, wakati vyombo vya habari vikipigwa marufuku Samunge, viongozi hao wamekuwa wakiwaita wanahabari kutoa taarifa mbalimbali wanazopenda kuhusiana na huduma ya Mchungaji huyo ikiwepo kusitishwa huduma kwa sababu mbalimbali, hali ya foleni na taratibu nyingine za tiba.
Mchungaji Mwaisapile, alianza kutoa tiba hiyo mwishoni mwa mwaka jana na vyombo vya habari ndivyo vilikuwa vya kwanza kuripoti tiba hiyo wakati Serikali ikipiga marufuku tiba hiyo kutolewa .(picha hiyo ya askali hapo juu haihusiani na tukio la habari hii-source Habari leo)
0 Comments