Uporaji wa mabilioni ya fedha kwa njia ya ujambazi katika taasisi za fedha umeanza kupungua na kuanza kukithiri kwa wizi huo katika taasisi hizo kwa kutumia teknolojia ya mtandao.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa Kimataifa na Mwakilishi wa Forensic CPA Society, ya USA, Sosthenes Bichanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Bichanga alikuwa akizungumzia mkutano wa pili wa kimataifa wa uhasibu wa kipelelezi Afrika unaotarajiwa kufanyika mjini hapa Mei 24 hadi 26, mwaka huu.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuwapatia watu ujuzi na uzoefu wa kupambana na wizi kwa njia ya mtandao kwa sababu siku hizi matapeli ni watu watanashati wasiotumia mabavu kuiba fedha kwenye mabenki.
“Watu wanatumia akili na sio mabavu…wizi wa kutumia mabavu sasa unaanza kupungua na badala yake wizi unaoshamiri kwa kasi ni wa kutumia teknolojia ya mtandao,” alieleza. Alisema taasisi nyingi za fedha hazipendi kuripoti matukio ya wizi yanayotokea kwa njia hiyo, pengine tu kwa kuona aibu.
Hata hivyo, alisema kwa kuendelea kukaa kimya bila kupiga kelele kwamba zinaibiwa, taasisi hizo zinashindwa kupata msaada wa kukabiliana na wizi wa aina hiyo, hali ambayo inawafanya wezi kuendeleza wizi wao kwa taasisi zingine.
Mkutano huo unaotawajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, utawashirikisha maafisa wa wizara hiyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), maofisa kutoka taasisi za fedha za umma na binafsi na wadau wengine wa fedha.
  (Sourse Nipashe)