Wananchi wanaokwenda katika kijiji cha Samunge-Loliondo wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha kwa ajili ya kupata tiba ya magonjwa sugu kutoka kwa Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila maarufu kama Babu, wameshauriwa kutoacha dawa, kupima afya zao mara kwa mara na kufuatilia maendeleo ya afya zao, badala ya kuridhika kuwa baada ya kikombe wamepona.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mwantumu Mwanko, alitoa ushauri huo jana wakati wa ufunguzi wa zoezi la kupima afya linalofanywa na Chama cha Madaktari Tanzania (Mati) Kanda ya Kaskazini mjini Moshi.
Alisema baada ya kupata kikombe cha dawa ya mchungaji huyo ambacho ni suala la kiimani zaidi, wagonjwa wengi hawarudi hospitali, lakini ni vizuri wagonjwa waliokuwa wanatumia dawa mbalimbali wakaendelea na dawa zao pamoja na kwenda kupima, ili kujiridhisha kuwa kweli maradhi yaliyokuwa yakimsumbua yameondoka na si kuendelea na mambo ambayo mgonjwa alikatazwa na daktari.
“Kutokana na sera ya serikali kila mmoja ni mdau wa afya, Mchungaji Mwasapila karuhusiwa kutoa huduma hiyo, lakini watu watambue kuwa kwa kawaida ugonjwa huingia haraka, lakini kupona kwake ni taratibu, hata kama dawa ya Babu inafanyakazi, lakini itachukua muda mrefu hivyo wagonjwa wa sukari, Ukimwi na shinikizo la damu wasiache dawa na wafuate mashatri waliyopewa hospitalini na pia wapime,” alisisitiza.
Dk. Mwanko alisema kupima afya ni muhimu kwa kuwa inasaidia kila mtu kujijua na jinsi ya kukabiliana na maradhi husika na kwamba maradhi yanasababisha kupoteza nguvu kazi na kwamba zoezi la upimaji afya linalofanywa na madaktari hao ni hatua nzuri katika kuwasaidia wananchi ambao wanatembea na maradhi bila kwenda hospitali.
Alisema kwa sasa Mkoa wa Kilimanjaro umeweka utaratibu wa kuwaelimisha wananchi waliokwenda kwa Babu na waliokuwa wameanza tiba za hospitali kuendelea na dawa na wale wote waliopata kikombe hufuatiliwa kwa karibu ili kuona kama wamepona maradhi yaliyokuwa yakiwasumbua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata), Dk. Zaitun Bokhary, akiwa daktari wa KCMC, wagonjwa wengi waliotoka katika hospitali hiyo kwenda kupata kikombe cha Babu hawakurudi kupima au kuendelea na matibabu waliyoanza, kitu ambacho alisema ni hatari.
Kiongozi wa zoezi la upimaji, Dk. Lairumbe Silangei, alisema madaktari wanaoendesha zoezi hilo ni kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga na kwamba linafanyika kwa mara ya kwanza na litakuwa endelevu kila mwaka ili kugundua magonjwa yanayowasumbua wananchi.
Alisema malengo ni kufikia watu 5,000 ambao watapimwa magonjwa ya sukari, shinikizo la damu, virusi vya Ukimwi na macho.
Watu watakaobainika kuwa na tatizo wataandikiwa kwenda katika hospitali za Mawenzi na KCMC.
“Zoezi hili linafanywa na madaktari kwa kujitolea. Hatuna mfadhili, lakini changamoto kubwa kwetu ni kama ukosefu wa vitendea kazi na vifaa vingine kuwa ghali mathalani kifaa cha kupima sukari…tumefanya hivi kwani tunajua maradhi yamesababisha kupungua kwa nguvu kazi katika kukuza uchumi, hivyo tunawasaidia wananchi,” alisema Dk. Silangei.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments