Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta, amesema Katiba itakayowawajibisha viongozi waliokabidhiwa madaraka ndio inayotakiwa kwa sasa nchini Tanzania, ili kufikia maendeleo ya kweli pamoja na kulinda amani na umoja uliopo.
Jaji Samatta ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza katika kongamano la katiba, lilofanyika chuoni hapo mkoani Morogoro.
Alisema katiba mpya inatakiwa ihamasishe uwajibikaji wa hali ya juu kwa watu watakaokuwa wamekabidhiwa madaraka.
Kongamano hilo la siku moja ambalo Jaji Samatta alikua mzungumzaji mkuu, lililokua na mada isemayo 'Changamoto katika Katiba ya sasa na mambo ya kuzingatia katika Katiba mpya', lilitayarishwa na Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Mzumbe na lilikua wazi kwa watu wote.
Alisema ni vyema Katiba mpya ikatoa nafasi ya uanzishwaji wa taasisi zitakazokuwa na jukumu la kuimarisha demokrasia nchini na kuchochea ukuaji wa demokrasia miongoni mwa vyama vya siasa.
Jaji Samatta, alisema katika kipindi cha karibu miaka 50 ya uhuru wa Tanzania, haijawahi kutokea kwa wananchi kushirikishwa moja kwa moja katika mchakato wa kutayarisha Katiba ya nchi ambayo ndio sheria mama. Akielezea changamoto za Katiba ya sasa alisema inasikitisha kwamba Katiba ya Tanzania haimtaji Mungu na kukubali nguvu zake. Alizitaja nchi za Uganda, Kenya, Ghana na Shelisheli kuwa zinamtaja na kukubali nguvu za Mungu katika Katiba zao.
Jaji huyo mstaafu, aliongeza kusema kuwa Katiba ya sasa pia haiwaenzi mashujaa wa taifa, ambao walijitoa kupinga uvamizi wa wageni na kupigania uhuru wa nchi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Magishi Mugasa, alisema kongamano hilo ni la muhimu hasa ikizingatia upeo mdogo wa wananchi kuhusiana na Katiba ya nchi.
“Wananchi wengi hasa wa vijijini hawafahamu kuhusu Katiba yetu, hivyo kongamano hili ni fursa ya pekee kwao kufahamu hili”, alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Chuoni hapo, Dk. Eleuter Mushi, alisema kiwepo kipengele kinachohusu umilikaji wa ardhi katika Katiba mpya, hasa kitakachoonyesha shughuli za serikali kuhusu ardhi na rasilimali nyinginezo ambazo itabidi zifanyike kwa kibali cha wananchi.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.
Washiriki walipata nafasi ya kuchangia maoni yao kuhusiana na mada husika, lengo kuu likiwa ni kuelimisha na kujadili changamoto mbalimbali zilizopo katika Katiba ya sasa na kupendekeza mambo ya kuzingatiwa katika Katiba mpya.
0 Comments