Baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya za mkoa wa Dar es Salaam wamejitosa katika sakata la kiuongozi ndani ya CCM mkoa wakiitaka Kamati Kuu ya CCM Taifa (CC), kuingilia kati na kutengua adhabu dhidi ya Mbunge wa Kinondoni Idd Azzan.
Adhabu hiyo iliyotolewa na CCM mkoa, ni pamoja na kumzuia Mbunge huyo kijana kugombea nafasi zozote katika chama hicho, pamoja na kujihusisha kwa namna moja ama nyingine katika masuala yanayohusu uongozi.
Wanachama hao pia walimtaka Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda na sekretarieti ya siasa ya mkoa huo kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Ilala Jumanne Kolekole, alisema anapinga uamuzi uliochukuliwa na Kilumbe Ng’enda dhidi ya Mbunge Azzan, bila kuwashirikisha wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Dar es Salaam.
Aliongeza kwamba mazingira ya sasa ya uendeshaji wa shughuli za CCM Dar es Salaam, yanawafanya baadhi ya wana-CCM kuanza kujiona kama wanatengwa kutokana na kushindwa kwa viongozi wa mkoa na hasa Katibu wake kuwashirikisha katika maamuzi yenye maslahi.
“Viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, wamekuwa wabinafsi na wenye kuona nafasi zao ni kama mamlaka isiyohitaji kuhojiwa na mtu ama mwanachama mwingine yeyote na ndio maana hata wakishauriwa jambo wanakuwa wakali na kuchukua hatua zikionyesha chuki,” alisema Kolekole.
“Mimi nadhani CCM Mkoa wa Dar es Salaam hauna viongozi wazuri, hawa akina Kilumbe na John Guninita (Mwenyekiti wa Mkoa) ni aina ya watu walioshindwa kazi na ambao kinachowafanya kuendelea na uongozi ni siasa za mazoea, na huyu ni mwenzetu na wala hawana sifa za uongozi,” alisema Mangundala.
Alisema wanaCCM wilaya ya Ilala wanaunga mkono kauli ya Mbunge Azzan ya kutaka viongozi wa mkoa na kwa kuanzia katika sekretarieti ya mkoa kuwajibika na kujivua gamba.
Kwa upande wa wilaya ya Kinondoni, baadhi ya wenyeviti wa CCM wa Kata hizo ambao hata hivyo waliomba kutotajwa majina gazetini, walisema kilichofanywa na uongozi wa CCM mkoa ni ubinafsi.
“Hawa viongozi wa mkoa ni wabinafsi sana, na kwa muda mrefu sasa wamekuwa na chuki binafsi dhidi ya Mbunge Azzan, na chuki zaidi ni baada ya jina lake kurejeshwa na Halmashauri Kuu ya Taifa NEC kuwa mgombea baada ya waliyekuwa wamemuandaa kutemwa Dodoma,” walisema.
Viongozi hao wa CCM pia walimtaka Mwenyekiti wa mkoa John Guninita kupima hali ya hewa na malalamiko yanayotolewa dhidi ya uongozi wake na akibaini mapungufu afuate mkondo huo kwa kuchukua hatua na kuwajibika wakiamini kwamba ameonyesha udhaifu katika uongozi.
Pia wamedai kwamba ameshindwa kuchukua hatua za kukemea kukua kwa makundi na uhasama ndani ya chama hicho tawala, huku makundi yaliyoibuka kabla na baada ya kura za maoni yakiendelea kukikosesha heshima chama kwa wananchi na wanachama wake.
Wilayani Temeke, wana-CCM nguli wa Kata za Yombo Makangarawe, Keko, Temeke, Kurasini walisema kilichofanywa na kamati ya Kilumbe ni hasira ya kuelezwa ukweli ambao viongizi wengi hawataki kuambiwa.
Hata hivyo, Kilumbe na Guninita walipotakiwa kulizungumzia suala hilo, walisema hata wao pia wanakiachia chama chao kuchukua maamuzi na ikiwa itabainika wamekosea kuchukua hatua watalazimika kuwajibika.
0 Comments