MTOTO wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama Bin Laden, Omar Bin Laden(pichani) amesema kitendo cha Marekani kuvamia nyumbani kwa baba yake na kumuua ni ujambazi hivyo anajipanga kutafuta haki katika Mahakama ya Kimataifa."Huu ni ujambazi usioweza kuvumilika. Ni ujambazi kwa sababu kuna vyombo vya sheria ambavyo angeweza kufikishwa na haki ikatendeka. Familia tunajipanga kudai haki mahakamani," alisema Omar.

Ametoa siku 30 kwa Serikali ya Marekani akisema kwamba zikipita bila kupata majibu ya kuridhisha, atafungua mashtaka kwenye mahakama ya kimataifa. Mtoto huyo wa Osama sasa anashauriana na mawakili wake
waliobobea, raia wa Uingereza kwa ajili ya suala hilo.

Omar alisema hayo katika taarifa yake iliyowekwa kwenye tovuti mbalimbali ambayo nakala yake ikaripotiwa na gazeti la New York Times jana.Katika taarifa hiyo iliyochapishwa na Gazeti la New York Times, Omar amehoji sababu za makachero wa Marekani kumuua baba yake badala ya kumkamata akiwa hai na kumfikisha mahakamani.

Mtoto huyo wa nne katika familia ya Osama alisema, yeye na ndugu zake wengine sasa wanaangalia taratibu za kisheria kuishtaki Marekani ili haki itendeke kutokana na mauaji hayo.
"Familia ina haki ya kudai haki ya baba yao. Tunaandaa taratibu za kisheria kuifikisha Marekani mahakamani ili mataifa yajue ukweli kuhusu tukio hilo," alisema Omar.

Katika taarifa hiyo, Omar pia alilaani kitendo cha Marekani kumzika baba yake baharini akieleza kuwa ni udhalilishaji kwake na familia.Aidha, ametaka ndugu zake waliokamatwa Mei 2, mwaka huu baada ya mauaji hayo, waachiwe huru baada ya kuendelea kuwaweka kizuizini na wakiteswa.

Ingawa taarifa hiyo haikuonyesha uhalisia kwamba imetolewa na Omar, watalaamu katika propaganda za kijeshi wamesema hawana shaka kuwa ni yake. Taarifa hiyo ilitolewa kupitia tovuti ya Islamist ideologue Abu Walid al-Masri.
Kusudio la Omar kuishtaki Marekani kwa mauaji ya baba yake limetolewa siku chache baada ya nchi hiyo kusema, itawaruhusu baadhi ya wanasheria kuangalia picha za maiti ya kiongozi huyo wa Al-Qaeda. Taarifa ya CIA imesema kuwa wanasheria hao wataona picha hizo kama watafika makao yake makuu.Bin Laden aliuawa na makachero wa Marekani Mei 2, mwaka huu nyumbani kwake katika mji wa Abbottabad, Pakistani.

Maofisa wa Marekani wameeleza kuwa makachero hao walilazimika kumwua Osama baada ya kuonekana kuwa amegoma kujisalimisha.
Katika hatua nyingine, kijana wa kiume wa bin Laden, Hamza (21) alitoweka wakati vikosi vya Jeshi la Marekani vilipovamia makazi alimokuwa akiishi baba yake na kumuua kwa risasi.Maofisa wa vikosi vya Usalama vya Pakistani walisema jana kuwa wanahofia kuwa huenda kijana huyo ambaye enzi za uhai wa baba yake alipewa jina la "gaidi mtoto" kutokana na ujasiri na utundu wake, amekwenda mafichoni kupanga mipango ya kulipiza kisasi.

Wake watatu wa bin Laden na watoto wake 16, wanashikiliwa na mamlaka za Pakistani baada ya uvamizi wa Marekani.
Taarifa hizo mpya zimetolewa wakati Marekani imeshafanya uvamizi na kumwua bin Laden huku Rais Barack Obama akisema walilazimika kutumia mbinu ya uvamizi ili kuepuka ukorofi wa askari wa Pakistani.
Hatua ya Rais Obama kupeleka kikosi maalumu chenye askari wengi Pakistani kimeonyesha kuwa alikuwa tayari kubeba mzigo wa lawama kwa kuivamia nchi hiyo bila kuitaarifu.
Taarifa za kutoweka kwa Hamza zilifahamika wakati wa mahojiano ya wake watatu wa bin Laden yaliyokuwa yakifanywa na makachero wa Pakistani.

Makachero hao walilieleza Shirika la Habari la ABC kuwa wake hao wa bin Laden waliwaeleza kuwa mmoja wa watoto wa kiongozi huyo Al Qaeda ametoweka na hajaonekana tangu wavamiwe katika makazi yao, lakini maofisa hao hawakuthibitisha ni mtoto yupi hasa.
Imethibitishwa kuwa kijana mwingine wa kiongozi huyo, Khalid (22) aliuawa na vikosi vya majeshi ya Marekani. Anaaminika kuwa mwili wake ni mmoja wa iliyokutwa katika makazi hayo baada ya shambulio na kisha kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya kurushia matangazo wiki iliyopita.

Awali, ilielezwa na Ikulu ya Marekani kuwa kijana huyo alikuwa akihofiwa kufa ingawa haikuwa na uhakika kuwa huenda alikuwa ndani ya kasri la baba yake, wakati walipovamiwa.Hamza alikuwa akichukuliwa na baba yake kama shujaa na mrithi. Aliwahi kuhusishwa na mauaji ya kiongozi wa Pakistani wakati huo Benazir Bhutto.

Makachero wa Pakistani wamekiri kupata taarifa za kutoweka kwa kijana huyo tangu Jumapili iliyopita. Ameshajitokeza angalau mara mbili katika picha za propaganda za baba yake, katika mkanda wa kwanza wa video uliotolewa mwaka 2001 pamoja na kaka yake Mohammed, Hamza alionekana akiwa amevaa magwanda akighani shairi.Katika moja ya mashairi hayo alighani akisema: "Ninawaonya Marekani kwamba watu wake watapata matatizo kama wakimsakama baba yangu. Kupambana na Wamarekani ndiyo misingi ya imani yetu."Mwaka 2005, wakati akiwa na umri wa miaka 15, alionekana kwenye mkanda wa video akiwa ameshika bunduki.