Mamalaka ya Mapato Nchini (TRA), imesema makusanyo ya kodi hayashuka kama inavyodaiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitlya, alisema kuwa makusanyo ya kodi nchini yameongezeka kwa asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka uliopita wa fedha.
Alisema katika kipindi cha Julai hadi Aprili mwaka huu wamekuwa wakikusanya wastani wa sh bilioni 430 kwa kila mwezi.
Alisema kwa takwimu zilizopo inaonyesha kuwa kila mwezi wamekuwa wakikusanya wastani wa sh bilioni 430.
Alifafanua kiasi hicho ni sawa na asilimia 93 ya makusanyo, ambapo ni pungufu ya asilimia 7 ya malengo yaliyokusidiwa.
Alisema mwaka huu wa fedha 2010/2011 wamepanga kukusanya sh trilioni 5.24
Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku (sio Nipashe), Zitto alikaririwa akisisitiza kuwa serikali haina fedha na kudokeza kuwa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mapitio ya uchumi ya mwezi Machi mwaka huu, inaonyesha kuwa imeshindwa kukusanya kodi kwa asilimia 15.
Alisema kuwa serikali imeshindwa kukusanya kodi kwa asilimia 15 isipokuwa ushuru wa forodha na hivyo haikufikia malengo ya ukusanyaji wa kodi.
Hata hivyo, hivi karibuni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alikanusha vikali taarifa iliyotolewa kwamba serikali imefilisika na hivyo kulazimika kukopa kutoka benki za ndani ili kugharamia mahitaji ya mishahara kwa watumishi wa serikali pamoja na posho mbalimbali za wabunge.
Alisema serikali inalipa watumishi wake mishahara kwa kutumia mapato yake ya ndani na pia ina uwezo wa kugharamia shughuli nyingine pamoja na gharama za kuendesha Bunge.
0 Comments