Mshiriki wa mashindano ya Big Brother Africa kutoka Tanzania, Lotus (pichani), ameenguliwa kutoka katika mashindano hayo na ametakiwa kuondoka mjengoni mara moja baada ya kumchapa kofi kijana wa Afrika Kusini, Luclay, jana asubuhi kufuatia ugomvi baina yao.

Lotus na Luclay waligombana ambapo awali walianza kwa majibizano na kisha kwa kivitendo, jambo ambalo Big Brother amesema mmoja wao angeweza kuondoka na kuepusha uhasama, kabla ya Lotus kumchapa kofi kijana huyo mwenye misuli.
Hali ilikuwa mbaya baada ya tangazo hilo ndani ya nyumba na kimwana wa Zambia, Kim, alikuwa akilia kwa sauti kubwa wakati wakimsaidia Lotus kufunga mabeki yake. Nic wa Kenya, Danny (Ethiopia), Karen (Nigeria), Mumba (Zambia) na Kim walimsaidia Lotus kufunga mizigo yake huku yeye akibaki mtulivu.
Kutokana na kuhusika kwake katika ugomvi, kijana Muafrika Kusini, Luclay, atachukua majukumu ya kuosha masufuria yote pamoja na kusafisha nyumba kwa kipindi chote atakachobaki ndani ya jumba. "Majukumu haya yatakuwa yako na yako peke yako. matendo yako dhidi ya washiriki wenzako pamoja na matamshi yako yatakuwa yakifuatiliwa wakati wote," Big Brother alimwambia Luclay.
Big Brother alieleza kwamba Lotus alivunja sheria ya mashindano ambapo adhabu ni kuondolewa mara moja mjengoni na kurudishwa nyumbani.
Tanzania imebaki kuwakilishwa na kimwana mwingine, Bhoke.