Wakimbizi wenye asili ya Burundi waliokuwa wakiishi katika makambi tangu mwaka 1972, watatawanywa kwenye mikoa 16 nchini ili kuwawezesha kuchanganyika na raia wengine.
Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa mkoani hapa, Athuman Akalama, aliwaambia madiwani wa halmashauri hiyo.

Alisema Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa 16 ambayo itawapokea wakimbizi hao waliojiandikisha kuwa raia wa Tanzania.
“Wilaya ya Kongwa imepangiwa kupokea kaya 700 na kutakiwa kuzitawanya katika vijijini mbalimbali,” alisema Akalama.
Alisema mkakati huo ambao unaojulikana kama mkakati wa utangamanishaji jamii, utakuwa wa miaka mitano na ulianza mwaka jana na kumalizika mwaka 2014.
Akalama alisema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, iliandaa semina ya kutambulisha mkakati huo na kwamba yaliyozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na mapendekezo ya wilaya katika utekelezaji wa mkakati huo.
Alisema mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza utoaji wa huduma za msingi kwa kila sekta ikiwemo mpango sambamba kwa makundi mahususi. Alisema katika mapendekezo hayo ya shughuli za maendeleo kwa sekta zote ambapo walipendekeza bajeti ya sh. bilioni 21.06.
Alisema katika ratiba ya utekelezaji wa mkakati huo, shughuli ya utoaji hamasa na maelekezo kwa ngazi zote za utawala yatazingatiwa. Alisema kabla ya kutambulisha mkakati huo katika baraza la madiwani, waliweza kutambulisha mkakati katika kikao cha menejimenti cha halmashauri hiyo, kamati ya mipango na fedha na kamati ya ushauri ya wilaya.
“Kwa kuwa semina ilikuwa ni hatua ya kwanza ya utambulisho wa mradi tunasubiri miongozo kwa maandishi itakayoelekeza utaratibu wa utekelezaji,” alisema.