Maelfu ya waandamanaji wamekesha katika medani ya kati ya mji wa Madrid ingawa mkusanyiko huo umepigwa marufuku na tume ya uchaguzi, kwa sababu ya uchaguzi wa majimbo wa hapo kesho.
Wimbi hilo la maandamano lilianza siku 6 zilizopita, na kusambaa katika miji kadha ya Uspania.

Maandamano yanaongozwa na vijana waliochoka na ukosefu wa ajira, ambao umefikia asli-mia-45% kati ya vijana, na rushwa na hisia kuwa wanasiasa hawawakilishi wao.
Mamia wameikalia medani ya Puerta del Sol kila siku, na wengine maelfu wanajumuika nao usiku.
Polisi wanasema waandamanaji elfu 25 walijaa katika medani na kufurika katika barabara za kando kando.
Saa sita za jana usiku, wakati amri ya kupiga marufuku maandamano hayo ilipoanza, umati huo ulikaa kimya kwa dakika, kisha ukaripuka kwa zomeo na kelele.
Tume ya uchaguzi ya Uspania ilitoa amri kuwa watu watawanyike jana usiku ili, "watu wapate muda wa kutafakari", kabla ya uchaguzi wa majimbo na serikali za mitaa utaofanywa kesho.
Lakini hadi sasa polisi hawakuingilia kati, na idadi ya waandamanaji inazidi kuongezeka.