Jamhuri ya Ireland inatekeleza operesheni kubwa zaidi ya kiusalama katika siku ya kwanza ya ziara ya Malkia Elizabeth nchini Ireland.
Ziara hiyo ni ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa Uingereza tangu jamhuri ya Ireland ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Uingereza miaka 90 iliyopita.
Malkia ataweka shada la maua kuwakumbuka wale walioaga dunia wakipigania uhuru wa Ireland.
Ziara hiyo ya malkia imesifiwa na kutajwa kama njia moja ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo ziara hiyo inafanyika huku visa vya mashambulizi ya kidini vikiendelea kuongezeka kaskazini mwa Ireland, mkoa unaozozaniwa na nchi hizo mbili lakini unathibitiwa na Uingereza.
Uingereza na Ireland ni mataifa mawili ambayo kwa muda mrefu yamegawanyika kutokana na maswala ya kihistoria.
Malkia Elizabeth wa pili anatarajiwa kuzuru maeneo ya kihistoria yanayozungukwa na utata, ikiwa na pamoja na uwanja wa Croke Park, ambako maelfu ya raia wa nchi hiyo waliuawa kinyama mwaka 1920 na bustani ya kumbukumbu mjini Dublin.
Maeneo hayo kama inavyoashiria majina yake, ni maeneo ya kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha yao wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa taifa hilo, wengi wao wakipambana na wanajeshi wa uingereza.
Dhamira kuu ya ziara hiyo ni kuonyesha kuwa nchi hizo mbili zimejikwamua kutoka kwa minyororo ya tofauti zao za miaka iliyopita.
Kwa upande mwingine ziara hiyo ya malkia itachochea hisia kali kwa wale wanaoamini kuwa utawala wa Ireland haupaswi kumualika kiongozi wa uingereza huku taifa hilo likiwa limegawanyika.
Raia wa nchi hiyo wamegawanyika kuhusu ziara hiyo.