MKUU wa Wilaya ya Kigoma, John Mongella amepiga marufuku usafirishaji wa mahindi nje ya wilaya hiyo.

Hatua hiyo inatokana na kukithiri kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaobeba mazao ya nafaka kwa kutumia malori kwenda nje ya mkoa wa Kigoma.


Akihutubia wananchi katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Chagu, Mtego wa noti, Ilolangula na Basanza, Mongella alisema vitendo hivyo ni balaa kubwa kwa siku zijazo kwa wananchi wa wilaya hiyo.


Alisema agizo hilo ni hadhari kwa kuzingatia hali ya ukame iliyoikumba wilaya hiyo mwaka huu.


“Mkoa wa Kigoma si miongoni mwa mikoa iliyo katika kundi la kupewa msaada wa chakula kutokana na hali nzuri ya hewa msimu wa kilimo uliopita lakini kasi ya uchukuaji nafaka inaweza kuleta matatizo,” alisema.
Aliwaagiza viongozi wa vijiji kuitisha mikutano ya vijiji na kuwaelimisha wananchi madhara ya kuuza chakula.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Adam Misana aliwataka wakulima kuhifadhi chakula kinachovunwa sasa kwa matumizi ya baadaye.


Misana alisema uzoefu unaonesha kuwa wakulima wengi huuza chakula chote na kisha kuhangaika.


Misana pamoja na mambo mengine alisema kitendo cha wakulima kuuza mazao yao sasa hakina faida kutokana na wanunuzi kuwanyonya kwa kuyanunua kwa bei ya chini.