MWALIMU Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi ya Nyalubanga, Zingula Omari (48) wilayani Geita amejeruhiwa kwa kukatwa panga ubavuni na kisha kufyekwa vidole usiku wa kuamkia jana na watu wasiojulikana.

Omari anadai chanzo cha uvamizi huo uliofanyika saa 7 usiku ni mgogoro wa eneo la shule hiyo iliyopo katika Kata ya Lwezera.


Akisimulia, alisema siku ya tukio akiwa amelala ndani ya nyumba yake katika Kijiji cha Lwezera, alivamiwa na watu asiowatambua baada kubomoa mlango kwa kutumia jiwe kubwa maarufu kama Fatuma.


Alisema baada ya kusikia mlango ukipigwa na jiwe hilo alinyanyuka na kukimbilia mlangoni, kisha kuusukuma kuwazuia watu hao wasiingie lakini akazidiwa nguvu.


“Baada ya kuuachia nilikimbilia chumbani kwa ajili ya kujificha. Walinifuata na kunieleza kwamba hawana shida yoyote nyingine tofauti na kuniua, ndipo mke wangu alipowauliza kwa nini wanataka kuniua hawakujibu na kuingia moja kwa moja chumbani na kunikata panga ubavuni,” alisema mwalimu huyo.


Alisema hata hivyo alijaribu kupambana nao kwa kulikamata panga lakini kwa bahati mbaya akawa amelikamata kwenye makali hali iliyomfanya mtu huyo aliyekuwa akipambana naye kulivuta na hivyo kumkata vidole vitatu vya mkono wa kulia na viwili vya kushoto.


Aliongeza kuwa baada ya kuona mapambano, watu hao walikimbia kabla ya majirani kukusanyika na kumpeleka katika zahanati kwa ajili ya matibabu ambapo ameshonwa ubavuni.


Akielezea chanzo cha kuvamiwa, Mwalimu Zingula alidai kumekuwepo ugomvi wa muda mrefu kati ya shule na mwanakijiji aliyehamia kijiji kingine.


Alidai uongozi wa shule akiwemo yeye waliamua kupeleka shauri hilo mahakamani kwa ajili ya kupata haki.


Kwa mujibu wake, siku aliyovamiwa ilikuwa aende katika Baraza la Ardhi kwa ajili ya kutoa ushahidi wa kesi hiyo.


“Walikuja kuniua kwa sababu kesho yake asubuhi nilikuwa nakwenda Geita mjini kwenye Baraza la Ardhi kwa ajili ya kutoa ushahidi na mimi ndiye mwenye ushahidi mkubwa kwenye kesi hiyo kwa sababu wakati eneo linachukuliwa na mtu huyo nilikuwepo kwa hiyo naona walitaka kuniua ili nisiende kutoa ushahidi kwenye kesi, namshukuru Mungu amenisaidia,” alisema.


Polisi wilayani Geita wamethibitisha kuwepo tukio hilo. Hata hivyo ilielezwa kuwa hadi juzi jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.


Hata hivyo taarifa kutoka katika jeshi hilo, zinasema uchunguzi unaendelea ikiwa ni pamoja na kumsaka mtu anayedaiwa kuwa na mgogoro na shule hiyo ili ahojiwe.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Maximillian Saasita licha ya kutoa taarifa Polisi, vile vile wameutaarifu uongozi wa Halmashauri ya Wilaya juu ya tukio hilo lililomkabili mtumishi.


Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu walimu wamekumbwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo huku baadhi wakitaka wahamishiwe maeneo mengine.