Zoezi linaloendelea la kukisafisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa njia ya kujivua gamba halitatekelezwa kwa kutumia ushahidi wa kimahakama dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema jana mjini hapa kuwa kinachofanyika chini ya zoezi hilo ni kwa makada wote, wakiwemo viongozi wa ngazi zote kujisafisha wao wenyewe kwa nia ya kujenga chama safi.
Vuai alisema hayo katika mahojiano na kituo binafsi cha Zenj FM kilichopo mjini Zanzibar.
Alisema CCM bado kinaamini kuwa rushwa ni adui wa haki na kwamba wanachama wote pamoja na viongozi wanaoamini katika dhana hiyo hivyo wanapaswa kuonyesha njia kwa kujivua gamba ili kuondokana na vitendo vya ufisadi.
“Wako wanaopenda rushwa na hawahitaji kusubiri ushahidi wa kimahakama, wao wenyewe wajikoshe ili chama kijijenge upya na wananchi waweze kukiamini,” alisema Vuai.
Alisema zoezi la kujivua gamba ni miongoni mwa maazimio 26 ya kukisafisha chama yaliyofikiwa Aprili 10 na 11, 2011 katika mkutano wa Halmashauri ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kupambana na ufisadi.(Source Nipashe)
0 Comments