Mvulana mwenye umri wa miaka 14, mkazi wa kijiji cha Senani kata ya Ipililo wilaya Maswa mkoani Shinyanga, amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kuchapwa viboko sita akiwa gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Maswa, Tamphon Mtani, alisema mshtakiwa huyo alikutwa na kosa la kumbaka mtoto huyo baada ya yeye kukiri kufanya na kutenda kosa hilo mbele ya mahakama hiyo.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Kidwadi Kalinga, aliiambia mahakama kuwa Mei 15, mwaka huu, saa 10:00 jioni, akiwa ndani ya nyumba anamoishi (ghetto) kijijini hapo, mtuhumiwa huyo alimwita mtoto huyo (jina limehifadhiwa) alipokuwa akicheza na wenzake jirani na nyumba hiyo.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa James alimwomba mtoto huyo aingie ndani ili ampatie pipi na ndipo mtoto huyo alipoingia hadi ndani ya chumba cha kijana huyo. Kwa mujibu wa Mwendasha Mashtaka, baada ya mtoto huyo kuingia chumbani, James kwa kudhamiria alimwingilia sehemu zake za siri mbele na nyuma na ndipo mtoto alipoanza kupiga kelele na majirani kusikia.
Alidai kuwa baada ya majirani kusikia na James kupata hofu, aliamua kukimbia kwa kutumia baiskeli, lakini wananchi walimhoji na kumuuliza kulikoni na walipoingia ndani ya chumba chake walimkuta mtoto huyo akitokwa damu sehemu zake siri na haja kubwa.
Wananchi hao walikwenda moja kwa moja polisi na ndipo mtuhumiwa alipokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kubaka na mbele ya hakimu huyo alipohojiwa alikiri kufanya kosa hilo. Hata hivyo, kijana huyo alipopewa nafasi ya kujitetea apunguziwe adhabu, hakufanya hivyo badala yake alibaki kimya.