Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema hali ya uchumi imezidi kuwa ngumu, huku bei ya vyakula ikizidi kupanda na vijana wakikosa ajira nchini.
Alisema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa Chama hicho Taifa, jijini Dar es Salaam jana, kinachofanyika siku mbili, kujadili hali ya siasa nchini, ‘Operesheni Zinduka’ namba mbili, kupokea ripoti ya namna serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar inavyoendelea, na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema hali hiyo inaendelea kuikabili nchi wakati alimkabidhi mkononi Rais Jakaya Kikwete nakala ya Ilani ya CUF ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana ili aipitie na kuona jinsi serikali inavyoweza kufanya ili kukuza uchumi wa nchi.
Lipumba, ambaye ni Profesa bingwa wa uchumi, alisema bei ya dhahabu imepanda kufikia dola za Marekani 1,800 (Sh. milioni 2.7) kwa wakia moja nje ya nchi, lakini hadi sasa serikali imeshindwa kunufaika na madini hayo.
Kutokana na hali hiyo, alishauri katika bajeti ya serikali ya mwaka huu wa fedha, kwenye sekta ya madini iwepo kodi maalum itakayoiwezesha serikali kupata walau asilimia 30 ya pato linalotokana na mauzo ya dhahabu nje ya nchi.
Alisema misamaha ya kodi inapunguza mapato ya serikali, hivyo akawataka wabunge kusimama kidete kuhakikisha wanadhibiti tatizo hilo.
Pia alishauri kutazamwa upya kodi ya mafuta ili isaidie kupunguza gharama za usafiri, ikiwa ni pamoja na kuondoa ukwepaji wa kodi ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa maisha.
Aliitaka serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kuwa na mipango inayotekelezeka, ikiwa ni pamoja na kutumia utulivu wa kisiasa ulioshamiri hivi sasa kutengeneza uchumi ili kuwapunguzia Wazanzibari gharama za maisha.
Aliishauri serikali kutotumia makosa ya kujikita katika kujadili mabadiliko ya Katiba pekee na kuacha kufanya maandalizi mapema ya kuwa na tume huru ya uchaguzi, ambayo alisema itasaidia kuepuka uchaguzi ujao wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuwa na mizengwe.
Alisema kadhia ya umeme ya sasa inasikitisha, kwani inashangaza kuona nishati hiyo ikitolewa kwa mgawo kutokana na kukosekana gesi, wakati nchi ikishindwa kutumia gesi asili iliyosheheni Mkuranga, Songosongo, Mnazibay na Pangani.
“Ukimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini maelezo yake, utasema ilifaa aongoze hii wizara kwa jinsi hoja zake zilivyo nzuri. Lakini Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, bado ni wale wale tuliotoka nao kwenye matatizo,” alisema Profesa Lipumba.
CHANZO: NIPASHE