POLISI mmoja amejeruhiwa pajani kwa risasi katika mapambano makali kati ya polisi na majambazi waliokuwa wanataka kuvamia mgodi wa dhahabu wa Nyamongo. Katika piga nikupige hiyo polisi walimjeruhi jambazi mmoja ambaye alitoroshwa na wenzake baada ya polisi kuwazidi nguvu. Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Rorya/ Tarime, Costantine Massawe alisema tukio hilo lilitokea Mei 5, mwaka huu katika Kijiji cha Nyakunguru, wilayani hapa. Katika tukio hilo polisi walifanikiwa kukamata bunduki mbili za vita aina ya Sub Machine Gun (SMG) zikiwa na risasi 23. Bunduki hizo zinasadikiwa kuwa miongoni mwa bunduki tano wanazodhaniwa kuwa nazo majambazi hao.
Kamanda Massawe alisema polisi walifanikiwa kugundua kuwepo kwa mpango huo wa majambazi hao kutaka kuvamia eneo la Mgodi wa Nyamongo na kuwahi eneo hilo na majambazi waliposhtuka walianza mapambano ya kukwepa kukamatwa. Imeelezwa katika patashika hiyo askari mwenye namba G.1932, PC Benny Antony (24), alijeruhiwa kwa risasi pajani na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu. “Tukio hilo lilitokea saa 10, alfajiri katika Kijiji cha Nyakunguru wakati askari wangu wakiwa doria katika maeneo hayo ambapo walikutana na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kuwataka kujisalimisha lakini watu hao walianza kuwarushia risasi askari.
“Kutokana na mashambulizi hayo ya ghafla askari wangu walianza kujibu mapigo ambapo PC Benny alijeruhiwa kwa kupigwa risasi katika mguu wake wa kushoto pajani na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Bugando kupata matibabu zaidi.”
Kamanda Massawe alisema katika mapambano hayo askari walifanikiwa kumjeruhi vibaya mmoja kati ya majambazi hao lakini wenzake walifanikiwa kutoroka naye kumuepusha na mikono ya polisi.
“Baada ya kukimbia askari waliona michirizi ya damu ikielekea katika maeneo ya kuingia katika Mto Tigite na kwenye misitu walikotokomea majambazi hayo,” alisema Kamanda Massawe.
Alisema polisi wanaendelea na msako wa majambazi hao ili kuweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda huyo alitoa mwito kwa wananchi mkoani Mara na nje ya mkoa huo kutoa taarifa mara moja katika vituo vya polisi vilivyo karibu nao watakapowaona watu wageni wakiwa na majeraha, ili kuwezesha kukamatwa kwa majambazi hao.
Matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yameanza kujirudia tena katika Wilaya ya Tarime . Hata hivyo Polisi imewataka wananchi kutoa taarifa mara moja kwa vyombo husika ikiwa ni pamoja na vituo vya polisi wanapowatilia shaka watu ili nyendo zao ziweze kufuatiliwa.
0 Comments