SAKATA la timu ya soka ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ kuja Tanzania kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, limemuibua Rais wa Shirikisho la Soka nchini hapa (Safa), akisema mchezo huo si sehemu ya kampeni zake.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Johannesburg, Rais wa Safa, Kirsten Nematandani, alisema si kweli kwamba anaitumia Tanzania katika kampeni zake za kuusaka ujumbe katika Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kama ambavyo imekuwa ikielezwa.
Nematandani alieleza kuwa hata safari ya Bafana Bafana kwenda Tanzania kuumana na Taifa Stars, haikuwa na mlengo wa kikampeni katika harakati zake, bali ilikuwa ni kuipa mazoezi timu hiyo kabla ya kuwavaa Wamisri mapema mwezi ujao.
Alisema hadhani kama anahitaji kusaidiwa katika kampeni zake za kuisaka nafasi hiyo ya ujumbe wa Caf, licha ya vyombo vya habari Afrika Kusini kudai kuwa anautumia ukaribu baina yake na Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Leodegar Tenga, kama nguzo kuu ya kueneza ushawishi wa kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
“Ni kweli hata mie nilienda Dar es Salaam pamoja na Bafana Bafana wakati wa mechi, lakini nilionana na Katibu Mkuu wa TFF pekee na lengo langu ilikuwa ni kuwatia moyo vijana,” alisema Rais huyo.
Hata hivyo bado vyombo vya habari nchini hapa, vinaendelea kudai kuwa Rais huyo anaitumia Bafana Bafana kutafuta ushawishi wa kuungwa mkono, na eneo lake kubwa analotegemea ni ukanda wa Afrika Mashariki na Kati akianzia Tanzania.
Madai hayo ya Bafana Bafana kutumika yamezidi kuchukua kasi baada ya Kocha Pitso Mosimane, kutangaza kikosi cha wachezaji 27 kuingia kambini kujiandaa kuwavaa Wamisri, huku kikosi hicho kikiwa na wachezaji saba pekee ambao walikuja Tanzania kukipiga na Stars.
Kikosi hicho cha Bafana kinaundwa na wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa Ulaya, huku wachezaji pekee waliokuja Tanzania ambao wanaweza kubakishwa katika safari ya Misri ni kipa Wayne Sandilands na mshambuliaji Katlego Mphela.
Hali hiyo inawafanya Waafrika Kusini kuendelea kuamini kuwa mechi ya Bafana Bafana naTaifa Stars haikuwa na maana yoyote kwa timu yao, na badala yake ikidaiwa kuwa na ajenda ya siri ndani yake.
Mechi hiyo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Stars ilifungwa bao 1-0.
0 Comments