WATU watatu wanashikiliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuiba mtoto wa mwezi mmoja na wiki moja.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Adolfina Chialo, amesema ofisini kwake jana kuwa, mtoto huyo

aliibwa juzi saa 2 asubuhi katika maeneo ya Chamwino mkoani humo.

Chialo alisema, Polisi walipata taarifa kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo, Prisca

Baltazary (20) mkazi wa Chamwino kuhusu kuibwa kwa mtoto huku akimtuhumu wifi
yake Salma Salum (25) kwa wizi huo.

Amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Antonia Kunja (25) na Mariam Kasim(25) wote

wakazi wa Chamwino mkoani Morogoro.

Inadaiwa kuwa, mama wa mtoto huyo alimpa Salma mtoto ili amshikie lakini baadaye wifi

huyo alimkabidhi mtoto huyo kwa binti yake wa miaka tisa na kumtuma dukani.

Binti huyo alipokuwa njiani, inadaiwa mama mmoja alijitokeza na kudai kuwa mtoto

huyo amebebwa vibaya na kuomba amsaidie kumuweka vizuri ndipo alipotokomea naye
kusikojulikana.

Kamanda Chialo alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi na watuhumiwa wanashikiliwa

kwa ajili ya uchunguzi zaidi.