SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema pamoja na kuwa na miradi yenye mikakati ya uhakika na wataalamu wa kutosha, bado linakabiliwa na ukata kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo itakayomaliza tatizo la umeme nchini itakapokamilika.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amewahakikishia Watanzania kuwa, Serikali ipo makini katika kukabiliana na tatizo hilo, na ifikapo mwaka 2013 kupitia miradi inayotekelezwa jumla ya megawati 1,000 zitaingizwa kwenye Gridi ya Taifa ya umeme.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya umeme nchini mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, amesema, kwa sasa urekebishaji wa mfumo wa umeme pekee unahitaji Sh trilioni 1.3.
“Ukweli ni kwamba tatizo kubwa tulilonalo ni fedha, tukisema tupandishe bei ya umeme, wabunge wanakuja juu, tukitaka kukopa fedha ni nyingi sana, lakini ijulikane kuwa mipango ipo na wataalamu wapo tatizo ni fedha na rasilimali,” amesisitiza Mhando leo.
Amesema, pamoja na hayo uwekezaji katika miradi ya umeme ni zaidi ya dola milioni 1,800 za Marekani ambapo aliitaja miradi iliyo tayari kutekelezwa kuwa ni Kiwira inahitaji dola milioni 400, usambazaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme zinahitajika dola milioni 700 na Kinyerezi dola za Marekani milioni 400.
Mhando amesema, kwa sasa shirika linazalisha kwa hasara kwa kuwa linatumia fedha nyingi kuzalisha na kutoza fedha kidogo kwa watumiaji na kila linapotaka kupandisha bei ya matumizi ya umeme, wabunge huja juu na kusababisha hali ya kifedha kuendelea kuwa mbaya.
Shirika hilo kwa sasa linatoza senti nane za Marekani kwa watumiaji wakati linatumia senti saba kuzalisha.
“Tungeomba sisi Tanesco tuachiwe huru bila kuingiliwa na wanasiasa katika utekelezaji wa masuala ya umeme, ukweli ni kwamba kwa sasa tunaingiza hasara ya Sh bilioni 58, kwa kuwa tunatumia fedha nyingi kuzalisha na tunaingiza kidogo,” amesema.
Akizungumzia hatua za dharura za kumaliza mgawo wa umeme sasa, alisema shirika liko kwenye hatua ya mwisho za kuchagua mzabuni atakayetekeleza mradi wa kukodi mitambo ya dharura itakayozalisha megawati 260.
Amesema, wameshamaliza utaratibu wa kutangaza zabuni na kampuni 15 zilijitokeza kuomba zabuni hiyo huku kampuni tatu tu zikijitokeza kurudisha maombi hayo na kati ya hizo tatu jana moja ilipatiwa tenda hiyo ya kutekeleza mradi wa kukodi mitambo ya dharura ambayo inatarajiwa kuzalisha rasmi umeme Julai, mwaka huu.
Aidha, Mhando amesema, mitambo ya Dowans ambayo sasa imenunuliwa na kampuni kutoka Marekani kuna uwezekano mkubwa ikanunuliwa na Serikali kutokana na mazungumzo yanayoendelea, jambo ambalo litawezesha kuongeza megawati 112.
“Ila kwa hapa tunasisitiza suala la taratibu za nchi kufuatwa kwanza kabla ya hatua yoyote.” Ngeleja alikiri kuwa hali ya umeme kwa sasa si nzuri na Serikali inajitahidi na imedhamiria kwa dhati, kuhakikisha kuwa tatizo hilo linaondoka nchini.
“Najua wapo watu wanaobeza juhudi za Serikali katika kushughulikia umeme, ndio changamoto zipo, lakini nawahakikishia Watanzania hadi 2013 hali hii itaanza kupungua.”
Akijibu hoja za Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Januari Makamba, kuhusu suala la mkataba wa Songas na Tanesco ambao unaonesha kuwa ipo mitambo minne inayoweza kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya ndege na gesi, alisema mkataba huo utachunguzwa na pande zote mbili zitakaa na kuangalia kama kuna upungufu.
Awali Makamba aliitaka Tanesco ijieleze ni kwa nini haikuchukua hatua dhidi ya Songas, kwa kuwa mkataba unaonesha wazi kuwa kampuni hiyo ina mitambo minne ya mafuta na gesi na sasa imezimwa kwa kuwa kuna upungufu wa gesi.
Wakati wa kujibu hoja hiyo Mhando alisema, hajausoma mkataba huo wa Songas na Tanesco, hali iliyosababisha Ngeleja kuingilia kati na kusema alisema ipo mikataba 24 ya kampuni hiyo na Tanesco na huenda Januari yuko sahihi na Songas pia, ndiyo maana kuna ulazima wa kuipitia upya mikataba hiyo.

0 Comments