MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) itaondoa magari yote yanayobeba abiria 30 na kuzuia watu binafsi kuendesha biashara ya daladala nchini, kwa lengo la kuboresha na kurahisisha usafiri huo.

Aidha, imesema itasimamia na kuhakikisha wanaopata leseni ya kuendesha biashara hiyo wanatimiza vigezo muhimu vitakavyoifanya kazi hiyo iheshimike na kuendeshwa kama fani nyingine kwa kuwa na madereva, makondakta na wasimamizi wenye ujuzi na elimu bora ya usafirishaji mijini na huduma kwa wateja.


Mpango huo, unaolenga kupunguza kwa asilimia kubwa wingi wa magari usioendana na uwezo wa barabara nchini, utatekelezwa ili pamoja na mambo mengine, umalize tatizo sugu la ukiukwaji wa sheria za usafirishaji abiria unaofanywa na madereva, makondakta na wamiliki wa vyombo hivyo.


“Hiyo hutokana na kiburi, dharau au kutokuwa na elimu kuhusu umuhimu wa huduma bora katika biashara hiyo na wamiliki sasa watalazimika kuwapa wafanyakazi wao mikataba,” imesema Sumatra.


Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray, alisema wameanza mchakato wa kuandaa taratibu sahihi za kubadili mfumo wa usafirishaji uliopo sasa kwenda mpya na kujipanga kutoa elimu kwanza kwa wasafirishaji mmoja mmoja, wanaoendesha biashara hiyo ili kuepuka migomo na vurugu zinazoweza kuibuka.


Kwa mujibu wa Mziray, mpango huo utatekelezwa miaka ijayo ambayo hata hivyo hakuitaja na utaruhusu kampuni au vikundi vikubwa vitakuwa na utambulisho wa kuwezesha Mamlaka hiyo kudhibiti kirahisi tofauti na ilivyo sasa.


“Kupitia utaratibu huo udhibiti utakuwa rahisi na utamgusa kila msafirishaji kwa kuwa utambulisho wao utakuwa ni kampuni au vikundi vikubwa tofauti na sasa ambapo wamiliki ni mmoja mmoja na ni wengi, kiasi cha kutukwepa na kuendesha biashara ya usafirishaji bila kuzingatia sheria.


“Watu wanaweza kudhani kuwa hatuwajibiki ipasavyo au kwamba tunafumbia macho makosa ya daladala, hiyo si kweli, kwa sababu changamoto hiyo inatusumbua sisi pia.


“Na ni vema watu wafahamu ukweli, kwamba kumdhibiti msafirishaji mmoja mmoja wa daladala ni kazi nzito kutokana na ujanja mwingi wanaoutumia”.


Amesema, wapo wamiliki wa daladala wanaodanganya anuani, namba za simu na wanadiriki kuziandika katika maelezo yao pindi waombapo leseni, jambo linaloifanya Sumatra ikwame kuwafikia magari yao yanapohusika na uvunjaji wa sheria .


Uvunjaji wa sheria ni pamoja na kukatisha njia, kuongeza nauli kiholela, kutoonekana barabarani kwa kipindi kirefu na kufanya kazi katika njia zisizo zao, kama inavyotokea kwa daladala za Posta-Mwenge, Kimara, Mabibo na nyingine ambazo hubadilishana njia kinyume cha sheria.


Alisema, daladala hizo zitakazoruhusiwa kutoa huduma hiyo mijini kwa kuanza na Dar es Salaam zinapaswa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 100 na zaidi kwa mara moja huku zikiwa na milango miwili kwa ajili ya abiria kuingia na kushuka, kuwa na vifaa vya kuhifadhia taka na huduma muhimu zinazomstahili abiria kulingana na nauli anayolipa.


Kwa maelezo yake, kutakuwa na ongezeko la nauli, hivyo Watanzania wajiandae kupokea huduma hiyo bora sambamba na ongezeko la nauli litakalotozwa kulingana na huduma.


Aliongeza, “Mipango ni kuchagua, usafiri bora na wa haraka ni gharama pia, hivyo Watanzania wajiandae kuupokea na kuridhika kuuchangia. Tutatoa elimu kwa wasafirishaji na watumiaji ili kuondoa usumbufu mara utekelezaji utakapoanza.”