Shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto, Save The Children, linasema kuwa watoto elfu-35 nchini Sudan wamelazimika kukimbia makwao kwa sababu ya mapigano katika eneo la mzozo la Abyei.
Abyei inaaniwa na Sudan Kusini na Kaskazini, na sasa inakaliwa na jeshi la Sudan Kaskazini.
Wakati huo-huo, Sudan Kusini inajitayarisha kujitenga na kaskazini mwezi wa July.
Fujo katika jimbo la Abyei zimezidi tangu mapigano yalipoanza mapema mwezi huu.
Save The Children inasema karibu wakaazi wote wa mji wa Abyei wamehama makwao, huku kukiwa na ripoti za mapigano, makaazi kuchomwa moto na uporaji.
Shirika hilo linakisia kuwa watoto 35-elfu wamekimbia na wengi wamepoteana na wazee wao.
Save The Children inasema iko tayari kusaidia lakini mapigano yanayoendelea yanazuwia msaada kufika katika maeneo yaliyoathirika.
Mwezi wa Januari watu wa Sudan Kusini walipiga kura kwa wingi kuamua kujitenga na Sudan Kaskazini.
Lakini kwa vile wanajeshi wa Sudan Kaskazini wameingia katika eneo la mpaka hilo la Abyei, taharuki imezuka tena katika nchi ambayo imekuwa ikijaribu kujikwamua kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo kadha.