SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema itaongeza mshahara kwa watumishi wa Serikali.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd wakati akihutubia kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani mjini Unguja.


“Niwaeleze tu kuwa mambo yatakuwa mazuri na tumbaku (fedha) itanoga kwa kiasi chake,” alisema Makamu wa Pili wa Rais huku akishangiliwa na wafanyakazi.


Alisema utafiti wa kitaalamu umefanywa ili kutoa mwongozo juu ya kima cha chini cha mshahara kitakachokidhi mahitaji ya maisha ya mfanyakazi wa Zanzibar kwa mujibu wa hali halisi ya maisha kwa sasa.


“Katika kufanya utafiti huo, watafiti wamekusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali pamoja na vyama vya wafanyakazi na jumuiya ya waajiri,” alisema Balozi Idd.


Alisema wakati Serikali inafanya juhudi ya kuboresha maslahi ya watumishi wote, ni muhimu wafanyakazi nao kuongeza bidii ya kazi.


“Nataka kila mfanyakazi amalizapo saa za kazi ajiulize kama kweli ametimiza wajibu wake ipasavyo…si vizuri kwa wafanyakazi kila siku kujitafutia dharura…leo mama mgonjwa, kesho babu mgonjwa, keshokutwa nakwenda harusini,” aliwaasa wafanyakazi.


Katika hatua nyingine, amevitaka vyama vya wafanyakazi kutowakingia kifua wafanyakazi wasio waadilifu, wabadhirifu, wazembe na wasio waaminifu pale waajiri wanapowachukulia hatua pamoja na kuwafukuza kazi kwa makosa ya aina hiyo.


Aidha, aliwaonya waajiri wenye tabia ya kunyanyasa wafanyakazi wakiwa kwenye Serikali au sekta binafsi kuacha mara moja unyanyasaji mahali pa kazi.


Makamu wa Pili wa Rais alisema vitendo hivyo havitavumiliwa na Serikali na kuwataka waajiri wote pamoja na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi kusimamia vyema sheria za kazi.


Katika kilele hicho cha Mei Mosi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi aliomba Serikali kuongeza maslahi ya Wafanyakazi kwa kuwa hali ya maisha inazidi kupanda.