Waziri wa Afya na ustawi wa jamii,Dr,Hadji Mponda kulia.

Serikali imesema kuwa katika bajeti ya fedha ya mwaka huu itaanza kusambaza vifurushi muhimu ambazo vitatumika kwa ajili ya akina mama wajawazito kujifungulia katika mikoa ya Dodoma na Pwani.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, alipokuwa akisoma hutuba kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete katika uzinduzi wa kampeni ya kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto (CARMMA).

Dk. Mponda alisema vifaa hivyo atapewa mama mjamzito wakati anapokuwa akihudhuria kliniki ili anapofikia muda wa kujifungua aende navyo hospitali.
Alisema vifaa hivyo vitakuwa vinatolewa bure na kwamba mpango huo utaanza kwa mikoa hiyo miwili na baada ya hapo utahusisha nchi nzima.
Hata hivyo, alisema Wizara yake ikishirikiana na wadau wengine imelenga kuboresha upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya huduma bora ya uzazi na mtoto katika hospitali 100 na vituo vya afya 200.
Dk. Mponda alisema kuwa mikakati hiyo inayofanywa na serikali ni kutaka kuboresha huduma za mama na mtoto katika suala la uzazi ili kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi.
Alisema pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo akina mama wajawazito kutojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, watoto kucheleweshwa kupelekwa kwenye vituo vya afya na wanaume kutoshiriki katika kupanga uzazi.