KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’, Jan Poulsen amemtwisha lawama mwamuzi Lamtey Joseph wa Ghana kwamba alisababisha timu yake isiibuke na ushindi katika mchezo wa juzi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mchezo huo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika mwaka 2012 ulifanyika mjini hapa na Stars kulala mabao 2-1, lakini Poulsen anawahurumia vijana wake kwani walipambana kwa nguvu zote na walistahili kuibuka na ushindi kama si mwamuzi huyo raia wa Ghana.
Kutokana na matokeo hayo ya juzi, Stars imejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu fainali hizo, kwani kama itahitaji kusonga mbele italazimika kushinda michezo yake miwili iliyobaki, huku ikiziombea mabaya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Morocco.
Morocco inaongoza Kundi D ikiwa na pointi saba sawa na Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini timu hizo zinatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Stars inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne sawa na Algeria inayoshika nafasi ya mwisho, lakini Stars yenyewe pia ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga. Morocco juzi iliifunga Algeria mabao 3-0.
Poulsen alisema vijana wake walicheza kwa nguvu, lakini mwamuzi hakutaka washinde, jambo ambalo lilimhuzunisha sana na kwamba mwamuzi huyo pamoja na waamuzi wasaidizi walikuwa ni wachezaji 12 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Alisema Stars haikucheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini walipoingia Athumani Machupa na Mbwana Samatta mambo yalibadilika, wakati waliposawazisha na kufunga bao la pili ambalo mwamuzi alilikataa.
Kuhusiana na matumaini ya Stars kufuzu fainali hizo, Poulsen alisema mazingira ni magumu kulingana na msimamo ulivyo.
Kwa upande wake kocha wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Jules Accrorsi aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo na kukiri kuwa haikuwa kazi rahisi kwao kushinda na kwamba walisahihisha makosa ya mchezo wao wa kwanza uliofanyika Machi 26 jijini Dar es Salaam ambapo Stars ilishinda mabao 2-1.
Katika michezo mingine iliyofanyika mwishoni mwa wiki, mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Misri walilazimishwa sare ya bila kufungana na Afrika Kusini mchezo uliofanyika Cairo, Misri, matokeo ambayo ni kama kuivua ubingwa Misri.
Misri inashika mkia kwenye kundi hilo ikiwa na pointi mbili na imebakisha mechi mbili, ambapo kama ikishinda zote itafikisha pointi nane, ambazo tayari inazo Afrika Kusini inayoongoza kundi hilo la G.
Kulingana na taratibu za mashindano hayo, mshindi wa kwanza katika kila kundi kati ya makundi 11 atafuzu fainali hizo, akiungana na wenyeji Equatorial Guinea na Gabon.
Timu nyingine tatu zitapatikana kulingana na timu zitakazokuwa na uwiano mzuri wa pointi, kwenye makundi yanayowania kufuzu fainali hizo, hivyo kupata idadi ya timu 16 zitakazocheza mashindano hayo mwakani.
Kwa mazingira hayo, ili Misri ifuzu itabidi ishinde mechi zote, huku ikiomba pia Afrika Kusini ifungwe na Niger Septemba, lakini kama Afrika Kusini ikifungwa inamaanisha Niger inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita itafikisha pointi tisa ambazo Misri haiwezi kuzifikia.
Pia mechi ya mwisho Afrika Kusini inacheza na Siera Leone, yenye pointi tano hivi sasa, ambapo kama Afrika Kusini pia itafungwa ina maana Sierra Leone itafikisha pointi nane ambazo ndiyo uwezo wa Misri kuzifikia. Kwa hesabu hizo Misri imevuliwa ubingwa.
0 Comments