Balozi wa Marekani nchini, Alphonso Lenhardt(Pichani juu), amewataka Watanzania kuwa wamoja na kuachana na tabia ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
Lenhardt alitoa ushauri huo jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za ubalozi huo alipokutana na baadhi ya viongozi wa dini.
Alisema dini ni kitu cha kuiweka jamii katika umoja na sio kuisambaratisha na kusema kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na misingi imara ya watu kuheshimiana kupitia dini zao.

Aliwataka viongozi wote wa dini zote kukaa pamoja na kujiona kama watu wamoja badala ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
Mmoja wa Watanzania waliokwenda nchini Marekani kwa ajili ya kujifunza mfumo wa kuabudu na watu kuheshimu dini za wenzao, Zaria Dunia kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), alisema kila Mmarekani ana haki ya kuabudu na kuheshimu dini ya mwenzake.
Zaria alisema akiwa nchini Marekani, alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo misikiti ambapo alisema Waislamu nchini humo wakishafanya ibada ya mchana wanapatiwa chakula kama njia ya kuwahamasisha kufika sehemu zao za kuabudu.
Alisema nchini Marekani hakuna chombo kinachoingilia uhuru wa mtu mwingine wala serikali yenye uwezo wa kuingilia dini ya mtu mwingine pamoja na uhuru wa kuabudu.
Aliwataka viongozi wa dini zote kubuni mbinu za kuwasaidia vijana wanaojihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya badala ya kuwaacha katika vituo vya mabasi kama ilivyo sasa.
Alifafanua kuwa nchini Marekani vijana kama hao wanasidiwa na viongozi wa dini badala ya kusubiri serikali ifanye kazi hiyo.
CHANZO: NIPASHE