Madam Ritta Paulsen,mkurugenzi wa Bench mark production inayoandaa Bongo Star Search.

Wakati pazia la Shindano la Bongo Star Search Second Chance limefunguliwa rasmi wiki hii, safu hii itawaletea wasomaji wetu mambo mbalimbali yanayojiri kila siku wakati wa shindano likiendelea.
Katika msimu huu wa tano, Shindano la BSS limekuja vingine kwa kuwapa nafasi ya pili washiriki waliotamba na kupendwa na mashabiki katika mashindano yaliyotangulia ya BSS kuwania tuzo ya mshindi wa kwanza.

Jumla ya washiriki 30 watashiriki katika mchakato wa kuwapata washiriki 20 watakaoingia ndani ya nyumba maalum ya "BSS Kili House" kwa ajili ya kuanza safari ya kuwania tuzo ya kinara wa BSS mwaka huu.
Historia ya shindano hilo iliyoanzia mwaka 2007, inaonyesha kwamba mshindi wa msimu wa kwanza alikuwa Jumanne Idd (2007), akifuatiwa na Misoji Nkwabi (2008), Pascal Cassian (2009) na Mariam Mohamedi alikuwa mshindi mwaka jana.
Katika zoezi la kuwapata washiriki hao, Watanzania wote watasaidiana na majaji kufanikisha zoezi hilo kwa kuwapigia kura watu wanaowaona wana vipaji na wanahitaji kuingia ndani ya nyumba ya BSS Kili House kwa ajili ya kuwania ushindi.
Katika muendelezo huo, leo tumeanza kuwachambulia majaji muhimu wa Shindano la BSS watakaokuwa na kazi kubwa ya kuwaongoza washiriki ili waende katika njia sahihi.

RITTA PAULSEN
Ritta Paulsen ni Mkurugenzi wa Kampuni ya BenchMark Production inayondaa Shindano BSS nchini.
Kazi ya ujaji aliianza mara shindano hilo lilipoanzishwa mwaka 2007, ambapo ametembelea sehemu mbalimbali nchini kutafuta vipaji.
Jaji huyu ambaye anajulikana kwa jina la 'Madame Ritta' mara nyingi anasema kazi ya 'kujaji' ni ngumu na inahitaji umakini na busara wakati wa kuamua.
Anasema, wakati wa 'kujaji' ni muhimu kuzingatia kipaji cha mtu, ubunifu wake na jinsi anavyoweza kubadilika kulingana na mazingira.
Ritta anasema kutokana na kuzingatia mambo hayo ndio maana BSS inaendelea kupendwa na kuthaminiwa na Watanzania wengi wakiamini shindano hilo linaweka daraja imara kwa vijana kusikika na kuonyesha vipaji vyao vilivyojificha.
“Ni kazi ngumu sana, inahitaji umakini wa hali ya juu ili kupata mtu aliye na kipaji kinachotakiwa, kutokana na vigezo hivyo tunaendelea kuaminiwa na Watanzania kwa kuona BSS ni sehemu ya kuwasaidia vijana,” anasema.
Madame Ritta ni jaji ambaye amekuwa kipenzi cha washiriki wengi kutokana na tabia yake ya kuwapa matumaini kila mara na kuwasaidia pale wanapohitaji msaada.
Kutokana na upendo wake kama mama ndani ya BSS, hufika wakati hutokwa na machozi wakati mshiriki anapotolewa.
“Katika kipindi cha kuwatoa washiriki nakuwa na wakati mgumu sana, huwa sina raha kabisa lakini kwa kuwa Watanzania ndio wanaoamua ninabaki kukubaliana nao,” anaongeza.
Kitu kingine alichonacho Madame Ritta ambacho wengi wamezoea kukiona ni tabia yake ya ucheshi.
Mara kadhaa akiwepo kwenye kiti chake cha ujaji huwa hajifichi tabia hii kwani wakati fulani anaonekana akiwatania majaji wenzake na hivyo kuleta burudani tosha kwa watazamaji.
Madame Ritta anasimama kama alama ya BSS kutokana na jitihada zake za kuendeleza vipaji vya vijana ikiwa ni pamoja na kuweka ubunifu katika kulifanya shindano hilo kuwa bora kila mwaka.
SURA MPYA
PAMOJA na matarajio mazuri katika BSS Second Chance 2011, Ritta alisema Watanzania watarajie kuona maamuzi mazuri wakati wa shindano hilo.
Alisema kitu kizuri katika mabadiliko wananchi wataruhusiwa kutoa maoni yao kwa kutumia simu, hivyo itasaidia yeye pamoja na majaji wenzake kuwa makini.
Aliwataka Watanzania waanze kuona maajabu ndani ya BSS kwa sababu wao ndio majaji wakuu wa kuamua nani mwenye kipaji na anaweza kuondoka na zawadi nono.
RITTA NJE YA BSS
Licha ya kuongoza vyema shindano la BSS, Ritta bado anakuwa mmoja wa wanawake mwenye wajibu wa kutunza vyema familia yake.
Akizungumza katika kituo cha televisheni cha EATV kupitia kipindi cha "Mwanamke Live" hivi karibuni, Ritta alisema pamoja na kuwa na mama wa mtoto mmoja, hakai chini na kwamba daima anaongeza juhudi katika kuhakikisha anafanikiwa maishani.
Alisema kuwa mama wa familia sio sababu ya kumfanya asijishughulishe katika kazi mbalimbali kama wanavyofanya wanaume.
“Mwanamke sio sababu ya kukufanya ukose fursa ya kufanya kazi, ni lazima kujiamini na kuona unaweza kwa kila jambo ndipo mafanikio yatakapokuja,” alisema.
Aliwataka wanawake kujikomboa kwa kujihusisha katika kazi za ujasiriamali pamoja na kuthubutu kuomba na kufanya kazi ambazo zinafanywa na wanaume.
Aidha, katika mambo anayoyapenda, Ritta alisema ni pamoja na sanaa ya urembo, kujisomea vitabu na kuangalia vipindi mbalimbali vya TV.