SERIKALI imetoa mwelekeo wa Bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2011/2012 na kutangaza kuwa shabaha yake kubwa itakuwa ni kumpunguzia mwananchi makali ya maisha ikianza na kushusha tozo za bidhaa ya petroli.
Hizo ni miongoni mwa hatua za haraka itakazochukua na Serikali katika Bajeti ijayo ili pia kuliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lipate fedha za kujenga mitambo ya kufua umeme.
Uamuzi huo ni kwa mujibu wa habari zilizopatikana ndani ya kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.
Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, anatarajiwa kutangaza uamuzi huo wa Serikali Jumatano wiki ijayo, wakati atakapowasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2011/12.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mkulo jana alitoa mwelekeo wa Bajeti hiyo kwa Kamati hiyo akisema uamuzi huo wa Serikali unalenga kupunguza ukali wa maisha ambao kwa sasa unamkabili mwananchi, kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa ikiwamo vyakula na zingine zisizo za chakula.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida jana Waziri Mkulo hakuwa tayari kuwaeleza waandishi wa habari mwelekeo huo wa Bajeti yake, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kila mwaka kabla ya Bajeti kusomwa.
Habari zilisema Mkulo alilielezea tatizo hilo kuwa ni changamoto kubwa kwa Serikali na akataka pia uungwaji mkono kutoka kwa wadau ikiwamo sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja.
Waziri alikiri kuwa, kupanda kwa gharama za maisha kumetokana na kupanda kwa bei za mafutana ukosefu wa umeme wa uhakika, hivyo Serikali ni lazima ichukue hatua za haraka kulishughulikia eneo hilo.
Pia alikiri kuwa licha ya sababu nyingi za kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, tozo nyingi kwenye bei ya bidhaa hiyo, nazo zimechangia nishati hiyo kupanda na kufikia lita moja ya petroli kwa sasa kuuzwa kati ya Sh. 2,060 na Sh 2,200.
Eneo hilo la tozo nyingi limekuwa likilalamikiwa na wananchi. Baadhi ya tozo zilizoko katika lita moja ya petroli ni za Mfuko wa Barabara, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kodi ya mapato, gharama za usafiri na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Taasisi nyingine zinazotoza mafuta na kuchangia kuongeza bei yake ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambao hata hivyo baadhi ya tozo hizo ni kwa fedha za kigeni hasa dola ya Marekani na nyingine ni kwa asilimia.
Katika maelezo yake, Mkulo alitaja sababu zingine za kupanda kwa bei ya mafuta kuwa ni kuongezeka kwa bima za meli kutokana na maharamia, uagizaji unaofanywa na kampuni moja moja na migogoro ya kisiasa inayoendelea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
“Serikali imepanga kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo katika tozo zilizopo katika bei ya mafuta,” alisema Mkulo katika kikao hicho.
Pamoja na hatua hiyo, Waziri pia aliiomba sekta binafsi iwezeshe upatikanaji wa huduma ya kutumia gesi kama nishati mbadala ya mafuta ya petrol, hasa katika maeneo ya mijini.
Kwa upande wa upatikanaji umeme, Mkulo alisema, Serikali inachukua hatua kuiwezesha Tanesco kupata fedha kutoka taasisi za kimataifa, kwa ajili ya kununua mitambo.
Lakini pia Serikali itaomba wananchi watumie kwa uangalifu umeme unaopatikana na pia wajielekeze zaidi katika matumizi ya umeme wa jua, wa upepo na unaotokana na nishati ya kinyesi cha mifugo.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando, aliiambia Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kuwa shirika lake lina hali mbaya na hivi sasa halikopesheki, hali inayolifanya lishindwe kutekeleza miradi yake ipasavyo katika juhudi za kutatua tatizo la umeme nchini.
Alilalamika kuwa Serikali haitoi fedha za kutosha kuliendesha na wakati huo huo likijiendesha kwa hasara.
Mkurugenzi huyo alisema, asilimia 70 ya mapato yao wanalipia umeme wanaonunua kutoka kampuni ya Songas na wakati hata umeme huo pia hautoshelezi mahitaji ya nchi.
Waziri Mkulo alitaja maeneo mengine ambayo bajeti hiyo itajikita zaidi mbali na umeme na kupunguza bei za mafuta, kuwa ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa kuimarisha bandari na barabara.
Sekta ya kilimo nayo imetajwa kuangaliwa zaidi hasa eneo la umwagiliaji na sekta ya maji na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Pia Mkulo alisema katika bajeti hiyo, Serikali inalenga kuimarisha hifadhi ya chakula kutokana na maeneo mengi kukumbwa na ukame.
Pia imepanga kuhamasisha wananchi walime mazao yanayostahimili ukame na wajenge utamaduni wa kuweka akiba ya chakula.
Pia eneo lingine ambalo Serikali itachukua hatua ya haraka ni la ajira ambalo ni tatizo kubwa sasa ambapo Mkulo alisema juhudi zinafanyika kuboresha ajira.
Alisema pia kuwa watafanya maboresho katika sekta ya fedha ili kutoa fursa ya wananchi wengi kupata mikopo ya mitaji ili waanzishe biashara.
Waziri alitoa mwito kwa mashirika ya umma, mifuko ya pensheni na sekta binafsi kuongeza fursa za ajira katika maeneo yao na kutoa mafunzo ya kujiajiri kwa wananchi.
Katika bajeti hiyo pia Waziri Mkulo alisema, Serikali inalenga kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha taratibu za fedha na ununuzi wa umma zinafuatwa kikamilifu.
Alisema wataboresha makusanyo ya ndani, watatilia maanani vitambulisho vya Taifa, kukusanya maduhuli kwa uhakika na kutenga rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa Mkukuta II.
Bajeti hiyo itakuwa ya Sh trilioni 13.5; kati ya fedha hizo Sh. trilioni 6.8 ni za ndani, Sh trilioni 3.9 za nchi rafiki wa maendeleo na Sh trilioni 2.5 mikopo kutoka vyanzo vya ndani na nje na Sh bilioni 812 ni mikopo mipya.
0 Comments