KAMA Kambi ya Upinzani Bungeni ingepewa fursa ya kuwasilisha Makadirio na Matumizi ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2011/12, basi katika mapendekezo yake ingetaka posho zote za vikao kwa watumishi wote wa umma wakiwamo wabunge zifutwe.

Hiyo imebainika katika maoni yake ya Bajeti ambayo yanayotarajiwa kusomwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo Juni 8 bungeni Dodoma.


Hata hivyo wabunge wa Kambi ya Upinzani, bado wanachukua posho hizo.



Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliwahi kudai kuwa mshahara wa Mbunge wa Sh. milioni 7 ni mkubwa huku akiuchukua, na baada ya kuacha ubunge, akaendelea kupata mshahara huo huo lakini kama posho ili asilipe kodi.


Kambi hiyo imesema ingependekeza pia kupunguzwa kwa bei ya mafuta kwa asilimia 40 ikiwa ni harakati za kumpunguzia mzigo wa maisha mwananchi wa kawaida.


Akiwasilisha vipaumbele vya bajeti hiyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo upande wa Fedha, Christina Lissu, alisema lengo la kufuta posho za vikao ni kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.


“Posho hizi kwa sasa ni nyingi na wakati mwingine wahusika hulipwa fedha nyingi kuliko hata mishahara yao. Sasa sisi tumeona kwa nini umlipe mtu fedha nyingine wakati akiwa kwenye vikao vya kazi, ambayo ni sehemu ya kazi na mshahara, haya ni matumizi mabaya ya fedha,” amesema Christina.


Aidha, alisema katika njia nyingine ambayo ‘bajeti’ hiyo imeainisha ya kuongeza mapato ya Serikali na kumpunguzia mwananchi wa kawaida mzigo, bei ya mafuta itapunguzwa kwa namna ambayo itampunguzia mwananchi mzigo wa mfumuko wa bei wa bidhaa muhimu vikiwemo vyakula.


Alisema, pia itahakikisha inapanua wigo wa kodi kwa kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 20 ya Pato la Taifa. Kwa sasa Serikali inakusanya mapato kwa asilimia 16 ya pato hilo, kuongeza wigo kwa walipa kodi na kupunguza msamaha wa kodi hadi asilimia moja kutoka 4.5.


Kwa upande wa kodi, bajeti hiyo imeonesha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zitatakiwa zijisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, ili kuiwezesha Serikali kuuza na kununua hisa na kuongeza mapato yake, ikiwa ni pamoja na kuweka sheria kali ya kuzuia ukwepaji kodi kwa mashirika makubwa.


Christina pia alitaja vipaumbele vingine vya bajeti hiyo kuwa ni pamoja na kipaumbele namba moja cha miundombinu, akisisitizia ujenzi wa barabara zote, kuboresha reli ya kati, bandari na kufufua Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATC).


Aidha, alisema kipaumbele kingine ni umeme kupitia uzalishaji wa makaa ya mawe ambao utazalisha megawati 1,500 kutoka migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira na gesi itakayozalisha megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza, ikiwa ni njia ya kupunguza utegemezi wa vyanzo vya maji.


Vipaumbele vingine ni kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini, maendeleo ya rasilimaliwatu kwa kuwekeza kwenye elimu na afya, ambapo kwa upande wa elimu, kodi ya uendelezaji ujuzi theluthi yake itabaki kwenye Bodi ya Mikopo badala ya kwenda Hazina.


Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha utawala bora kwa kuanzisha ofisi ya kushughulikia mafisadi wakubwa ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma.