Jengo la Baraza la Wawakilishi Zanzibar lililoanza kutumika Januari mwaka huu, limeanza kuvuja na kusababisha serikali kuamua kufanya tathimini ya kiwango cha ubora wake.
Utekelezaji wa kazi ya ujenzi na usimamizi wa jengo hilo ulifanywa na Kampuni ya Al-Youseif Chantable Society, ya Saud Arabia na kukabidhi jengo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Agosti mwaka jana.

Uchunguzi  umebaini kuwa sehemu kadhaa za paa la jengo hilo zilianza kuonekana zinavuja Machi mwaka huu, ikiwa ni miezi nane tu, tangu ujenzi kukamilika kwa gharama ya Sh.bilioni 3.5.
Mkuu wa Idara ya Utawala, Mipango na Raslimali watu wa BLW, Mdungi Makame Mdungi, amethibitisha kuwa jengo hilo linavuja na kwamba wakandarasi wametarifiwa juu ya tatizo hilo.
Alisema wahandisi wa Al-Youseif Chantable Society tayari wamefanya kazi ya awali ya kukagua sehemu zinazovunja.
“Wahusika wametaarifiwa juu ya hali hiyo na tayari wamefika kukagua maeneo yenye matatizo,” alisema.
Alisema mradi wa ujenzi wa jengo hilo ulikuwa umekabidhiwa serikalini baada ya kukamilika, lakini kupitia muda wa uangalizi wa mradi huo, serikali bado ina nafasi ya kuwabana wahusika kuwajibika kwa matatizo yanayojitokeza.
Mdungi alisema mvua za masika zilipoanza, ndipo jengo hilo la ghorofa moja likabainika linavuja.
Ujenzi wa jengo hilo umegharamiwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya Al-Youseif, ambayo imetoa asilimia 50 ya gharama za ujenzi na SMZ italipa asilimia 50 ya gharama hizo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Aboud Mohamed Aboud, alipohojiwa alisema, “tayari nimepokea taarifa kutoka kwa katibu mkuu wa wizara yetu.”
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo hatua zinazochukuliwa na wizara yake ni kuwasiliana na wahandisi wa idara ya ujenzi Zanzibar ili wafanye tathimini ya kulikagua jengo hilo.