Mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Nigeria amekamatwa na polisi wa kupambana na ufisadi.
Spika wa bunge la wawakilishi linalomaliza muda wake Dimeji Bankole alizuiliwa kuhusiana na madai ya ubadhilifu wa mamilioni ya dola,fedha za serikali.
Alikamatwa baada ya makao yake katika mji mkuu Abuja kuzingirwa.
Atakamatwa
Alipoapishwa kuchukua madaraka wiki iliyopita, Rais Goodluck Jonathan aliahidi kukabiliana ufisadi uliokita mizizi nchini Nigeria.
Mwandishi wa BBC Jonah Fisher anasema kukamatwa kwa Bw Bankole si suala ambalo halikutarajiwa, baada ya wiki kadhaa za tetesi zilizochapishwa katika magazeti ya nchi hiyo kwamba atakamatwa.
Msemaji wa tume ya kukabiliana na uhalifu wa kiuchumi na kifedha nchini humo(EFCC),alisema kuwa tume hiyo ilipokea taarifa kwamba Bw Bankole alikuwa akipanga kutoroka nchini.
Shutma
Sawa na wabunge wengine, muhula wa Bw Bankole unamalizika Ijumaa- na bunge jipya linatarajiwa kuapishwa Jumatatu.
Alipoteza kiti chake katika uchaguzi wa mwezi Aprili.
taarifa ya EFCC inasema Bw Bankole anatafutwa kujibu shutma zinazomkabili.
Miongoni mwa shutma hizo ni pamoja na matumizi mabaya ya dola milioni 60, na kuchukua dola milioni 65 kama mkopo binafsi akitumia akaunti ya bunge kama dhamana.
Awali msemaji wa Bankole Idowu Bakare, alitoa taarifa akisema kuwa "hakuwahi kunufaika" kwa kutumia nafasi yake. Liliripoti shirika la habari la AP.
0 Comments